Rais Steinmeier amwagia sifa waziri mkuu Ethiopia
29 Januari 2019"Nimefika katika nchi iliyobadilika, nchi inayochipuka. Nchi inayofanyiwa mageuzi. Kwa niaba ya wote niliofuatana nao, naamini nnaweza kusema tuna fakhari na kusifu moyo wenu wa ujasiri wa kuanzisha mageuzi kama haya."
Amesema hayo rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier baada ya mazungumzo pamoja na rais wa Ethiopia bibi Sahle-Work Zewde mjini Addis Abeba.
Rais Steinmeier amekutana pia na waziri mkuu Abiy Ahmed anaewekewa matumaini makubwa na sio tu nchini Ethiopia.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 42 ndie aliyeanzisha mageuzi hayo makubwa tangu April mwaka 2018. Amewaachia huru maelfu ya wafungwa wa kisiasa na kuanzisha mfumo wa kiliberali wa kiuchumi.
Waziri mkuu Abiy Ahmed amefikia makubaliano ya amani pamoja na nchi jirani ya Eritrea wanakotokea wakimbizi wengi wanaoingia Ujerumani. Amefanikiwa pia kuleta wezani wa kijinsia katika nyadhifa za serikali.
Changamoto bado zipo lukuki
Hata hivyo bado mivutano ya kikabila inatishia umoja wa nchi hiyo. Umaskini na ukosefu wa ajira ni wa hali ya juu.
Ethiopia inakabiliwa na changamoto kubwa-kisiasa, kiuchumi na kijamii, amesema rais Steinmeier aliyehakikisha ni kwa masilahi ya Ujerumani kuona mageuzi yanafaana na kuahidi Ujerumani itasaidia kwa uwezo wake wote mageuzi nchini Ethiopia.
"Nuru ya mapambazuko ya kidemokrasi inaweza kunawiri mpaka nje ya Ethiopia hadi barani Ulaya na kwa namna hiyo kuibadilisha pia picha ya Afrika barani Ulaya, picha inayoliangalia bara la Afrika kuwa ni bara la mizozo na mivutano.
Ujumbe wa wanauchumi unafuatana na rais Steinmeier katika ziara yake hii ya siku nne nchini Ethiopia. Jumatatu jioni rais Steinmeier na ujumbe wake wamepangiwa kutia saini waraka wa ushirikiano kati ya kampuni ya Volkswagen na tume ya vitega uchumi ya Ethiopia. Lengo ni kubuni chombo cha usafiri kwaajili ya nchi hiyo yenye wakaazi milioni 100.
Rais Steinmeier amepangiwa kukutana na viongozi wa Umoja wa Afrika siku ya Jumatano.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa
Mhariri: Grace Patricia Kabogo