Rais Sisi wa Misri aondoa hali ya hatari kwa mara ya kwanza
26 Oktoba 2021Misri ilitangaza hali ya hatari Aprili 2017 baada ya miripuko ya bomu makanishani na imekuwa ikiirefusha kila baada ya miezi mitatu, licha ya kuimarika kwa hali ya usalama.
Al-Sisi ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa Misri imekuwa eneo salama na la utulivu katika kanda hiyo na ndio maana imeamuliwa kwa mara ya kwanza katika miaka mingi kufuta urefushwaji wa hali ya hatari katika maeneo yote ya nchi.
Hali ya hatari iliwapa maafisa nchini humo mamlaka makubwa ya kuwakamata watu na kuwakandamiza wale iliowaita maadui wa taifa.
Mwanaharakati maarufu wa Misri Hossam Bahgat ameikaribisha hatua hiyo akisema itazuia matumizi ya mahakama za dharura za usalama, ijapokuwa haitatumika kwa baadhi ya kesi kubwa ambazo tayari ziliwasilishwa katika korti za aina hiyo.