1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Salva Kiir na Riek Machar washindwa kukubaliana

7 Machi 2015

Mswada wa ripoti ya Umoja wa Africa, wapendekeza Sudan Kusini isimamiwe na jumuiya ya kimataifa na viongozi wa pande zinazopigana wapigwe marufuku kushiriki katika siasa.

https://p.dw.com/p/1Emyq
Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo alieongoza tumea ya uchunguzi
Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo alieongoza tume ya uchunguziPicha: Getty Images

Katika mswada wa ripoti yake,Umoja wa Afrika umetoa mwito wa kuiweka Sudan Kusini chini ya usimamizi wa jumuiya ya kimataifa.Umoja wa Afrika pia umependekeza katika ripoti hiyo kwamba Rais wa sasa Salva Kirr na kiongozi wa waasi Riek Machar wapigwe marufuku kushiriki katika shughuli za siasa.

Rais Salvar Kirr na Machar wanahusika moja kwa moja na machafuko

Nakala ya ripoti hiyo ya Halmashauri ya Umoja wa Afrika juu ya uchunguzi uliofanywa nchini Sudan Kusini, iliyopatikana na shirika la habari la AFP, inawalaumu Rais Salva Kirr na kiongozi wa waasi Riek Machar kwa kuhusika moja kwa moja na siasa chafu zilizosababisha vita.

Südsudan-Verhandlungen vorerst gescheitert
Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek MacharPicha: Reuters/Tiksa Negeri

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo alieingoza tume ya uchunguzi aliiwasilisha ripoti hiyo kamili mnamo mwezi ya Januari lakini haikuchapishwa kwa sababu ya kuhofia kuyahujumu mazungumzo ya amani. Mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa upatanishi wa Jumuiya ya kiserikali ya mandeleo ya nchi za mashiriki mwa Afrika, IGAD, yalivunjika hapo jana (Ijumaa) mjini Addis.

Umoja wa Afrika unaweza kuingilia kati

Rais Salva Kirr na kiongozi wa waasi Riek Machar walishindwa kufikia mapatano ya kugawana madaraka katika muda wa hadi alhamisi iliyopita uliowekwa na wapatanishi. Wanadiplomasia wamedokeza kwamba mapendekezo yaliyomo katika mswada wa ripoti ya Obasanjo yanaweza kuweka msingi wa mazungumzo juu ya njia ya kuuwezesha Umoja wa Afrika kuingilia kati kwa uthabiti, nchini Sudan Kusini

Lazima Salva Kirr na Riek Machar waenguliwe

Ripoti hiyo inasema jambo muhimu, katika juhudi za kuleta haki, katika kipindi cha mpito nchini Sudan Kusini, ni kuwaweka nje ya nyadhifa za juu, wale wanaohusika na umwagikajidamu wa kiwango kikubwa, kutokana na mapigano yaliyoanza tarehe 15 mwezi Desemba mwaka 2013. Hata hivyo, siyo viongozi wa Sudan Kusini pekee wanaobeba lawama juu ya mgogoro wa nchi hiyo. Serikali za nchi za kanda na jumuiya ya kimataifa na hasa Uingereza, Norway na Marekani pia zinabeba lawama juu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 yaliyokuwa yamekaa kombo.

Südsudan-Verhandlungen vorerst gescheitert
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Reuters/Jok Solomun

Mkataba wa mwaka 2005 ulikuwa kombo

Makubaliano hayo ndio yaliyovimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya Kaskazini na Kusini vilivyochukua miaka mingi. Lakini makubaliano hayo pia yalilipa jeshi la waasi uongozi wa Kusini. Ripoti ya Umoja wa Afrika imesema kuwa mkataba wa amani wa mwaka 2005 ulianzisha nchini Sudan Kusini, mamlaka ya kisiasa ambayo hayakuweza kupingwa - mamlaka ya watu walioweza kutenda uhalifu bila ya kuwajibishwa, na hivyo kuhalalisha utawala wa bunduki.

Tume ya Umoja wa Afrika imeshauri kwamba Sudan Kusini isimamiwe na pande tatu: Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na jopo la kimataifa na hivyo kuweza kuwaweka wanasiasa wasiowajibika nje kabisa ya uongozi wa nchi.

Mwandishi: Mtullya Abdu/afpe,rtre,

Mhariri: Bruce Amani