1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Saied amteua Waziri Mkuu mwanamke Tunisia

29 Septemba 2021

Rais wa Tunisia Kais Saied amemteua Najla Bouden Romdhane,kuwa Waziri Mkuu mpya. Romdhane ambaye ni mtaalamu wa maswala ya jiolojia na mhandisi katika chuo kikuu hana uzoefu juu ya mambo ya kiserikali.

https://p.dw.com/p/413Ln
Tunesien Tunis Präsident Kais Saied und neue Premierministerin Najla Bouden Romdhane
Picha: Tunisian Presidency/REUTERS

Rais wa Tunisia amemteua mwanamke huyo wa kwanza kushika wadhfa wa Waziri Mkuu takriban miezi miwili baada ya kujipa nguvu zote kama raisi katika hatua inayotajwa na wakosoaji kuwa ni mapinduzi.

Najla Romdhane, Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Tunisia, amepewa jukumu na rais Kais kuunda serikali haraka iwezekanavyo.

Ofisi ya rais imetoa mkanda wa vidio unaomuonesha kiongozi huyo wa nchi akikutana na Waziri Mkuu Bouden ofisini mwake, na kummpa jukumu hilo la kuja na serikali mpya ndani ya saa au siku zijazo. Bouden anaingia afisini wakati ambapo nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi.

Rais amesema jukumu kubwa la serikali ijayo ni kukabiliana na rushwa na mivutano inayoendelea katika taasisi nyinyi za serikali ya Tunisia.

Watunisia wasema hawaoni mabadiliko maishani mwao

Tunesien Tunis politische Krise | Proteste gegen Präsident Kais Said
Raia wa tunisia wakiandamana kupinga hali mbaya ya maisha nchini mwaoPicha: ZOUBEIR SOUISSI/REUTERS

Bouden aliye na miaka 63 atakuwa Waziri mkuu nambari kumi kuteuliwa tangu mwaka 2011 wakati wa maandamano ya kudai mabadiliko yalimuondoa madarakani dikteta wa muda mrefu  Zine El Abedine Ben Ali.

soma zaidi: Rais wa Tunisia aahidi kutaja jina la waziri mkuu mpya

Nchi hiyo imesifika kimataifa kwa namna ilivyopitia kipindi cha mpito kwa njia ya kidemokrasia, lakini watunisia wengi wanasema hawaoni mabadiliko maishani mwao na wamekwama na serikali isiyofanya kazi wa raia wake iliyojaa rushwa. 

Mwezi Julai rais Kais Saied aliifuta serikali ya Waziri Mkuu wa zamani Hichem Mechichi, kuvunja bunge, na kuchukua mamlaka baada ya miezi kadhaa ya mkwamo wa kisiasa kufuatia mgogoro wa kiuchumi na vifo zaidi vitokanavyo na virusi vya corona.

Wiki iliyopita alijipa nguvu zote kama rais na amekuwa akikabiliana na miito tofauti inayomlazimisha kuunda serikali.

Chanzo: reuters,afp