1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Rouhani wa Iran ziarani nchini Uturuki

9 Juni 2014

Rais wa Iran anafanya ziara ya siku mbili Uturuki katika wakati ambapo nchi hizo mbili zinajaribu kuimarisha uhusiano wao licha ya mashindano ya kuania ushawishi wa kimkoa na hitilafu za maoni kuhusu mzozo wa Syria.

https://p.dw.com/p/1CEpR
Rais Hassan Rouhani wa IranPicha: Irna

Rais Hassan Rouhani aliyefuatana na ujumbe mkubwa wa serikali yake amepangiwa kukutana na maafisa wa serikali ya Uturuki,ikiwa ni pamoja na rais Abdullah Gul na waziri mkuu Recep Tayyeb Erdogan mjini Ankara.Mada mazungumzoni zitahusu usalama pamoja pia na biashara kati yao.Iran na Uturuki zimepangiwa kusimamia kwa pamoja kikao cha kwanza cha baraza la ushirikiano-taasisi iliyoanzishwa na Ankara kwa lengo la kuhimiza biashara ya kimkoa..

Kabla ya kuondoka Teheran,rais Rouhani alinukuliwa na shirika la habari la Iran-Irna akisema atalizusha pia suala la Syria pamoja pia na lile la Irak wakati wa mazungumzo yake pamoja na viongozi wa mjini Ankara.

Hali ya mambo katika eneo la Afrika kaskazini,Palastina na mashariki ya Kati nayo pia itajadiliwa.

"Ni muhimu kuzungumzia masuala yote hayo pamoja na Uturuki" rais Rouhani amenukuliwa na shirika rasmi la habari la Iran-Irna akisema na kusisitiza "kuimarishwa uhusiano wa pande mbili "ni muhimu kwa eneo lote hilo."

Biashara ya pande mbili itaimarishwa

Ziara ya rais Rouhani mjini Ankara inatokea muda mfupi tu tu kabla ya mazungumzo ya ana kwa ana ya mjini Gevena kati ya Iran,Marekani,na Umoja wa ulaya kuhusu mradi wa nuklea wa Iran.

Erdogan Khamenei Iran Türkei
Waziri mkuu Erdogan alipoitembelea Iran mwishoni mwa mwezi wa januari mwaka huuPicha: Mehr

Rais Rouhani anatarajiwa kutia saini makubaliano yatakayoimarisha uhusiano pamoja na Uturuki-uhusiano uliodhoofika kutokana na vita nchini Syria ambako serikali ya Iran inaiunga mkono serikali ya ya rais Bashar al Assad huku Uturuki ikiwaunga mkono waasi.

Makubaliano ya kiuchumi na hasa ushirikiano katika sekta ya nishati,gesi na umeme yanatarajiwa kutiwa saini.

Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyeb Erdogan alifika ziarani nchini Iran januari mwaka huu.Wakati ule alizungumzia azma ya kuzidisha kiwango cha biashara ya pamoja kati ya nchi zao mbili toka dala bilioni 13.5 mwaka 2013 na kufikia dala bilioni 30 ifikapo mwaka 2015.

Ikitegemea kwa sehemu kubwa nishati kutoka Iran na Urusi,Uturuki inapanga kuzidisha kiwango cha mafuta na gesi kuoka Iran pindi vikwazo vya kimataifa vikiondolewa,makubaliano yatakapofikiwa kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran mjini Geneva.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman