Rais Vladmir yuko tayari kukutana na Donald Trump
28 Machi 2018Wakati huo huo balozi wa Urusi nchini Australia amesema dunia inaweza kuingia katika hali ya vita baridi ikiwa mataifa ya magharibi yataendeleza chuki dhidi ya Moscow.
Kwa mujibu wa msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, "Putin yuko tayari na Urusi yenyewe iko tayari kuendeleza mahusiano ya pande mbili kwa kulingana na uaminifu wa kila nchi, ikiwemo Marekani."
Marekani na zaidi ya mataifa mengine 20 yalitangaza wiki hii kwamba yanawafukuza wanadiplomasia wa Urusi katika kile kinachoonekana ni kushikamana na Uingereza, katikati mwa mzozo baina ya mahasimu hao wa zamani wa vita baridi. Peskov amebainisha kuwa wanataraji mataifa yaliyoungana na Uingereza kufikiria upya juu ya uamuzi wao.
"Tuna matumaini kwamba nchi zilizonyesha mshikamano na Uingereza na kuchukua uamuzi wa kufukuza wanadiplomasia wetu, zitatafakari tena jinsi habari hizo kama za kuaminika, ambazo zinawasilishwa kama ushahidi wa ushiriki huu wa kisiasa wa Urusi katika matukio ya Salisbury," alisema Peskov.
Naye balozi wa Urusi nchini Australia amesema hii leo kwamba dunia inaweza kujikuta imetumbukia katika "hali ya vita baridi" ikiwa mataifa ya magharibi yataendelea na chuki yake dhidi ya Moscow katika kukabiliana na shambulio la sumu ya mishipa ya fahamu dhidi ya jasusi wa zamani wa kisovieti na Uingereza.
Balozi Grigory Logvinov ameyaonya mataifa ya magharibi wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Canberra akisema, "Sasa ni juu ya mataifa ya magharibi kuacha na kuelewa kwamba kampeni dhidi ya Urusi haina mustakabali mzuri wa baadaye".
Wakati huo huo Slovakia imesema itawaita mabalozi wake wa Urusi ili kutafuta ushauri juu ya madai ya sumu na kusema kwamba itachukua hatua kali, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya kigeni wa taifa hilo Moroslav Lajcak.
Taifa hilo la Ulaya ya kati halijaungana na mataifa mengine 19 pamoja na Marekani na Australia katika kuwatimua wanadiplomasia wa Urusi. Balozi huyo amesema katika taarifa yake kwamba, "serikali imeunga mkono mapendekezo ya kuwaita mabalozi kwa ushauri. Ni hatua kubwa za kidiplomasia, hatujawahi kumrejesha balozi katika kipindi cha miaka 25", Miroslav amewaeleza waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa kawaida wa serikali.
Uingereza tayari imewatimua wanadiplomasia 23 wa Urusi juu ya tukio hilo, na Urusi yenyewe ilifuata mkondo na kuwafukuza idadi sawa ya wanadiplomasia.
Uingereza inadai kwamba Urusi ilitumia silaha ya kemikali kumshambulia jasusi wake wa zamani amabye pia alikuwa jasusi wa Urusi huko mashariki wa Uingereza mapema mwezi huu. Urusi sasa inazingatia namna ya kukabiliana na wimbi la kufukuzwa kwa wanadiplomasia wake, ambalo mwanadiplomasia wa juu wa Moscow Sergei Lavlov ameituhumu Marekani.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/Reuters
Mhariri: Josephat Charo