Rais Ouattara wa Ivory Coast kukutana na hasimu wake Gbagbo
27 Julai 2021Rais wa Ivory Coast Alassane Quattara leo anakutana na hasimu wake Laurent Gbagbo aliyefutiwa mashitaka ya uhalifu wa kivita na mahakama ya kimataifa ya ICC. Mkutano wa leo umezusha sintofahamu katika mji mkuu wa Abidjan, lakini katikati mwa wasiwasi huo kunaonekana kuwepo na matumaini miongoni mwa raia wengi.
Ouattara alikubali hadharani kurejea kwa Gbagbo. Alitumia sherehe ya Waislamu ya Eid al-Adha kutoa wito wa mshikamano wa kitaifa akisema kuwa "hatua zilizochukuliwa za mshikamano wa kijamii, maridhiano, ziendelee kuchukuliwa. Raia wa Ivory Coast waendelee kuishi katika amani".
Msemaji wa Gbagbo alisema kuwa mahasimu hao wawili wamekuwa "katika mawasiliano" ya simu tangu mwanzoni mwa mwezi Julai. Ingawa, mkutano wa mwisho wa hadhara baina ya Ouattara na Gbagbo ulikuwa wakati wa uchaguzi wa rais wa mwaka 2010 ambao ulizozaniwa. Hadharani, viongozi wote wawili wameashiria taswira ya amani na maridhiano. Baadhi ya raia wa taifa hilo wana matarajio yafuatayo
"Ninachofikiria kuhusu mkutano wa rais Gbagbo na rais Alassane, ni kwamba hawa ni ndugu. Wote watauonyesha ulimwengu kwamba kuna maridhiano hapa Ivory Coast".
"Ninadhani kwamba mkutano baina ya rais Gbagbo na rais Alassane unaashiria siku nzuri kwa sababu yetu watu wa kaskazini na kusini kwamba bado kuna matumaini."
Wakati tume huru ya uchaguzi ilipomtangaza Ouattara kuwa amemshinda Gbagbo katika uchaguzi unaotambuliwa na Umoja wa Mataifa, nchi hiyo ilitumbukia katika ghasia. Kutoaminiana kati ya jamii za kaskazini, zinazomuunga mkono Ouattara na jamii za kusini za washirika wa Gbagbo kuliongezeka. Gbagbo alikataa kukubali kushindwa na baraza la katiba linalodhibitiwa na Gbagbo lilisema matokeo ya urais yalikuwa batili na likatangaza matokeo mapya yaliyompa ushindi Gbagbo wa asilimia 51.45.
Gbagbo alikataa kuondoka na yakazuka mapigano yaliyowaua watu 3,000 baina ya wapiganaji wa Gbagbo na vikosi vya Ouattara vilivyokuwa vikiungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS na vikosi vya Ufaransa. Baadhi ya asasi za kiraia kama Femmes de Salem zimejaribu kuhimiza maridhiano kwa jamii zilizoathirika na machafuko yaliyochangiwa na uchaguzi wa mwaka 2010.
Kwa raia wengi wa Ivory Coast, kumalizika uhasama baina ya rais Ouattara mwenye umri wa miaka 79 na Gbagbo mwenye umri wa miaka 76 ni suala la muhimu sana katika kuondokana na mizizi ya mzozo katika nchi hiyo.