Rais Obama nchini Ujerumani
19 Juni 2013Ratiba yake
Obama amepangiwa pia kukutana na Kansela Angela Merkel na kuhutubia pia maelfu ya watu katika lango la Brandenburg ambako anatarajiwa kuitolea mwito Jumuiya ya Kimataifa kutia bidii katika kuzishughulikia changamoto za dunia.
Rais barack Obama aliwasili katika ikulu ya rais Gauck kwa mazungumzo na rais huyo, kwa gari aina ya Limousine iliyopachikwa jina la The Beast,chini ya ulinzi mkali akisindikizwa na msafara wa pikipiki.
Rais Obama aliwasili tarehe 18.06.2013 nchini Ujerumani na kulala katika hoteli mjini Berlin akitokea katika mkutano wa kundi la nchi tajiri kiviwanda la G8 uliomalizika Jumanne huko Ireland kaskazini.
Ikiwa ni takriban miaka 50 tangu rais wa zamani wa Marekani John F. Kennedy alipotowa hotuba yake na kutangaza'' Ich bin ein Berliner yaani mimi ni mkaazi wa Berlin'' na miaka 26 tangu Ronald Reagan kutoa mwito wa kuvunjwa ukuta wa Berlin,Obama atasimama palepale katika lango la kihistoria la Brandenburg kutangaza mipango ya kupunguzwa kwa theluthi moja silaha za Kinuklia za wakati wa vita baridi.
Mada za mazungumzo
Rais huyo wa Marekani pia atafanya mazungumzo na Kansela Angela Merkel ambaye kawaida anamuheshimu sana katika uhusiano wao.Hata hivyo katika mkutano na Merkel Obama atakuwa chini ya shinikizo kubwa la kumtaka aeleze juu ya umbali iliofikia mipango ya kijaasusi ya Marekani ya shirika lake la usalama wa taifa la NSA ambayo inatajwa imekuwa ikikusanya data kuanzia za simu hadi mitandao ndani ya Marekani na katika nchi za nje.
Merkel ameshasema atahitaji uwazi kutoka kwa Obama na kuongeza kwamba wajerumani wanahitaji kufahamu ikiwa mienendo yao katika mitandao imekuwa ikifuatiliziwa na NSA. Aidha katika hotuba yake kwenye eneo hilo la kihistoria Obama anategemewa kupendekeza hatua ya kupunguza silaha za kivita za Nuklia,mpango huo utazihitaji Marekani na Urusi kila mmoja kupunguza kiasi silaha 1000 za Nuklia,huku pia akiiomba , Ulaya kupunguza silaha zake za Kinuklia.
Hata hivyo haijawa wazi ikiwa rais wa Urusi Vladmir Putin ambaye amekuwa na majadiliano makali na Obama nchini Ireland ya Kaskazini siku ya Jumatatu,atakubaliana na mpango huo wa Obama.Awali itakumbukwa Urusi ilitaka pafanyike mabadiliko katika mfumo wa ulinzi wa makombora kabla kuiwafiki agenda hiyo ya Nuklia.
Halikadhalika Obama ataweka wazi nia yake ya kuhudhuria mkutano wa kilele kuhusu usalama wa Nuklia utakaofanyika The Hague mwaka ujao pamoja na kutangaza kuandaa mkutano wake juu ya suala hilo mwaka 2016 ambao ni mwaka wake wa miwhso madarakani.Hotuba yake hiyo itakayotuwama zaidi katika suala la Nuklia inalenga kuhakikisha kwamba suala la kupambana na uenezaji silaha za Nuklia linabakia kuwa agenda yake muhimu katika sera zake za Nje.Marekani inamiliki kiasi silaha 20 za kivita za Nuklia ambazo bado zimewekwa Ujerumani.
Wakati wa kuanguka ukuta wa Berlin mwaka 1989 nchi hiyo ya Marekani ilikuwa na kiasi silaha 200 za Nuklia za kivita ndani ya Ujerumani.Rais Obama bado anapendwa na wajerumani,kwa mujibu wa utafiti wa maoni uliofanywa wiki hii na gazeti la die Zeit unaonyesha asilimia 60 ya wajerumani wameridhika na jinsi anavyoongoza.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo