1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama awasilisha mpango wa kufufua uchumi

9 Septemba 2011

Rais wa Marekani Barack Obama amewasilisha mpango unaoazimia kufufua uchumi na kutoa nafasi mpya za ajira na utakaogharimu dola bilioni 450.

https://p.dw.com/p/Rkhr
President Barack Obama delivers a speech to a joint session of Congress at the Capitol in Washington, Thursday, Sept. 8, 2011. Watching are Vice President Joe Biden and House Speaker John Boehner. (Foto:Kevin Lamarque, POOL/AP/dapd
Rais Barack Obama akihotubia bunge mjini Washington, Marekani.Picha: dapd

Katika hotuba yake hiyo iliyokuwa ikingojewa kwa hamu, Obama ameliambia bunge, lengo ni kufufua uchumi wa Marekani uliozorota, kutoa nafasi mpya za ajira na kuwapa vijana matumaini.

Kiini cha mpango huo ni kupunguza gharama za ruzuku ya serikali kwa wale wasiojiweza na kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu na miundo mbinu. Lengo pia ni kufanya mageuzi katika mfumo wa kodi, ili wenye pato kubwa kabisa wasiwe wenye kunufaika zaidi. Kinachohitajiwa amesema, ni mfumo utakaohakikisha kodi ya haki kwa kila mmoja. Obama vile vile, amependekeza kupunguza kodi ya pato kwa nusu. Hata kampuni zipunguziwe kodi ili ziweze kutoa nafasi mpya za ajira au kuongeza mishahara ya wafanyakazi wake.

Rais Obama ameliomba bunge kuuidhinisha mpango huo. Amesema, Marekani hivi sasa ikikabiliwa na mzozo wa kitaifa, Warepublikan na Wademokrat hawana budi kuwajibika.