1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama ameanza vipi kazi Ikulu ?

Ramadhan Ali22 Januari 2009

Nini hatima ya gereza la Guantanamo na wafunga wake ?

https://p.dw.com/p/GeAi
Rais Barack ObamaPicha: AP

Safu za leo za wahariri wa magazeti ya Ujerumani, zimechambua zaidi mada mbili:Kwanza, jinsi rais Barack Obama alivyoanza kazi yake baada ya kutawazwa na pili, hatima ya gereza la Guantanamo baada ya amri yake ya kusimamisha kesi kwa muda wa siku 120 na mwishoe, kufungwa kabisa.

Ramadhan Ali amewakagulia safu hizo na kwanza analikamata gazeti la OLDENBURGISCHE VOLKSZEITUNG:

"Wanasiasa wa Ulaya, wanatumai sasa kuwa,kwa kubadilika kwa uongozi Marekani,kutafungua mlango wa ushirikiano barabara. Iwapo matarajio hayo yatatimilia,soma juu ya mfano anaotoa Barack Obama katika mkasa wa gereza la Guantanamo.Lakini katika swali la kuwapokea wafungwa watakaotolewa kutoka gereza hilo la Guantanamo, yaonesha kunatokota mvutano.

Waziri wa ndani wa Ujerumani Wolfgang Schauble, hakukosea kudai swali hilo ni shughuli inayoihusu Marekani tu.Vipi aonavyo Obama, haijulikani."

Ama Braunschweiger Zeitung linaona kwamba ulimwenguni kote rais Barack Obama anapigiwa makofi akishangiriwa kwa kuachana na siasa ya nguvu-nguvu ya kijeuri aliyofuata mtangulizi wake.salamu za mapenzi kutoka Moscow lakini zimesikika kimya kimya.Gazeti laongeza:

"Rais Dimitri Medwedew wa Urusi na waziri wake mkuu Wladmir Putin, wameamua kunyamaa kimya,hatahivyo,wako tayari kukaribisha mwanzo mpya katika uhusiano wao.

Moscow ingeliweza kutumia kutawazwa rais kwa Obama kubainisha utayarifu wake wa kukaribisha mageuzi."

Rais Obama hataki kuifanya Marekani kuwa polisi pekee wa dunia bali ni azma yake kuzijumuisha nchi nyengine za kidemokrasia za magharibi kujitwika nazo jukumu lao. Katika jukumu hilo,gazeti la Kolnische Rundschau linadai :

Kanzela Angela Merkel anarudi nyuma....kwavile kila mara akikariri na kusisitiza jinsi Ujerumani ilivyochangia wanajeshi wake nchini Afghanistan.Anatoa ishara wazi:zaidi Ujerumani haiwezi kubeba."

Gazeti la Neue Presse kutoka Hannover, linampongeza rais Obama likisema hapotezi wakati kwani, mara tu baada ya kukaa kitini amesimamisha kwanza kesi na amechukua hatua za kwanza kulifunga kabisa gereza la Guantanamo,kisiwa Kuba. Gazeti lakini lauliza:wale wafungwa wasio na hatia waliopo katika gereza hilo wafanywe nini-wale ambao hawawezi kurejeshwa makwao ?

Mada hii inajadiliwa wakati huu huku Ulaya.Hatahivyo, ni jukumu la rais Obama kufumbua kitandawili hiki,kwani, ni Marekani iliowanyakua binadamu hao na kuwapeleka huko.Kutumai mwishoe, kitandawili hiki kitapata ufumbuzi mzuri,huenda kwa kushika hatamu rais Obama.