Rais Obama akutana na Netanyahu na Abbas
22 Septemba 2009Mkutano huo wa pande tatu unaofanywa siku moja kabla ya kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hautazamiwi kuleta tija, hasa Israel ikiashiria tangu mwanzoni kuwa haipo tayari kubadilisha sera za ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.
Kwa maoni ya vyombo vya habari vya Israel, mualiko uliotolewa na Rais wa Marekani Barack Obama kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel ni ufanisi kwake kwani kabla ya kwenda mkutanoni mjini New York, hajakubali kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya yanayokaliwa na Israel . Wakati huo huo ofisi ya Netanyahu imesema, wakati wa mkutano huo wa pande tatu, Netanyahu atatetea sera za serikali yake kuhusu ujenzi wa makaazi hayo. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Danny Ayalon amesema:
"Umuhimu wa mkutano huo ni ukweli kuwa mkutano huo unafanyika. Jitahada thabiti za Marekani zimevunja nguvu msimamo wa Wapalestina."
Amesema, kama Mahmoud Abbas alifikiria kuwa ataitumia serikali mpya ya Marekani kuishinikiza serikali ya Israel ,basi sasa ametambua kuwa serikali hiyo haikushtushwa wala haikubadilisha msimamo wake.
Kuambatana na mpango wa amani maarufu kama "Road Map" uliokubaliwa mwaka 2003, Israel inatakiwa isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi katika maeneo inayoyakalia ikiwemo pia Jerusalem ya Mashariki. Na Rais wa Wapalestina alisisitiza hayo alipozungumza na waandishi wa habari.Amesema:
"Ikiwa Israel inataka kufanya majadiliano basi lazima isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi na baadae ndio tutajadili masuala yaliyo muhimu."
Hamas wanaodhibiti Ukanda wa Gaza wanamlaumu kwa mara nyingine tena Rais Mahmoud Abbas kwa kutoheshimu ahadi alizotoa. Licha ya madai,kutaka ujenzi wa maeneo ya Wayahudi usitishwe moja kwa moja kabla ya kushiriki katika mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa Israel, amekwenda New York kwa mazungumzo hayo hayo. Waziri mkuu wa zamani wa Palestina Ismail Haniyeh amesema huko Gaza, si PLO ya Mahmoud Abbas na wala si chama kingine chenye haki ya kudhuru mwongozo wa umma wa Palestina.
Mwandishi:C.Verenkotte/ZPR/P.Martin
Mhariri: M.Abdul-Rahman