1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama akutana na Mfalme Abdullah

Halima Nyanza18 Mei 2011

Rais Barack Obama wa marekani amesema machafuko ya kisiasa yaliyozikumba nchi za kiarabu ni muhimu zaidi katika kufufua mazungumzo ya amani yaliyosimama kwa muda mrefu kati ya Israel na Wapalestina.

https://p.dw.com/p/11Ils
Rais Barack ObamaPicha: AP

Akizungumza baada ya mazungumzo yake na Mfalme Abdullah wa Jordan, ikiwa ni mwanzo wa mchakato wa kidiplomasia katika Mashariki ya Kati, Rais Barack Obama wa Marekani ameahidi kuendelea kushinikiza ufumbuzi wa kuwepo kwa mataifa mawili katika mzozo huo wa Palestina na Israel licha ya kushindwa kwa juhudi zake hizo mpaka sasa.

Jordanien König Abdullah II Kabinett Umbildung
Mfalme Abdullah wa pili II wa JordanPicha: AP

Amesisitiza kuwa machafuko yanayotikisa eneo hilo kwa sasa yanatoa nafasi kwa Waisrael na Wapalestina kuanza tena mazungumzo yaliyovunjika mwaka jana kutokana na mvutano juu ya ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika ukingo wa magharibi.

Hata hivyo, Rais Obama ambaye anatafuta kujiunganisha tena na ulimwengu wa kiarabu, hakutoa mawazo mengine yoyote mapya juu ya kuendelea kwa mchakato wa amani.

Amekuwa akijitahidi kubadili msimamo wa waraabu kwa kuiona Marekani kama nchi isiyochukua hatua za haki katika mkakati wake wa kutafuta amani kati ya Israel na Paslestina.

Rais wa Marekani ambaye kesho pia amepanga kutoa hotuba kuhusiana na machafuko yanayotokea katika nchi za kiarabu, atakutana pia Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Ijumaa na kuihutubia jumuia inayounga mkono Israel siku ya Jumapili.

Katika hatua nyingine, Rais Obama amekuwa na matumaini kutumia mauaji ya kiongozi wa mtandao wa la Qaeda Osama bin Laden, ambayo kwa sasa yameimarisha msimamo wake nchini mwake na nje ya nchi yake, kama nafasi ya kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na waraabu.

Viongozi hao wawili wa Marekani na Jordan katika mazungumzo yao pia wametafuta muafaka wa pamoja juu ya machafuko yaliyozikumba nchi za kiarabu, ambayo yamesababishwa kuondolewa madarakani kwa viongozi madikteta waliokuwa washirika wa Marekani katika nchi za Misri na Tunisia na pia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya.

Rais Obama ameahidi pia kuipa Jordan kiasi ya dola bilioni moja mahsusi kuifadhili miradi ya maendeleo.

Jordan pia ilikabiliwa na upinzani wa kutaka kumpunguzia madaraka mfalme wa nchi hiyo, ambapo mfalme wa nchi hiyo mwezi Machi alimfukuza Waziri wake mkuu na kuahidi kufanya mabadiliko ya katiba.

Machafuko mengine pia yametokea katika nchi za  Syria, Yemen na Bahrain.

Mwandishi: Halima Nyanza( Reuters)

Mhariri:  Yusuf Saumu