1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

090511 Obama Pakistan

9 Mei 2011

Rais wa Marekani, Barack Obama ameongeza shinikizo dhidi ya Pakistan akiitaka kuwatafuta waliomsaidia kiongozi wa al Qaeda aliyeuwawa, Osama bin Laden.

https://p.dw.com/p/11BvM
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: AP

Rais Obama ameiambia televisheni ya CBS ya Marekani kwamba lazima kulikuwa na mtandao uliomsaidia kiongozi huyo nchini Pakistan, vinginevyo hangeweza kuishi kwa miaka mingi mjini Abottabad, mji ambao una kambi kadhaa za jeshi la nchi hiyo. Kwa rais Obama, ni wazi kwamba Osama bin Laden lazima alikuwa na mtandao uliomsaidia. Hata hivyo serikali ya Marekani mpaka sasa haifahamu mtandao huo wala nani aliyemsaidia kiongozi huyo wa al Qaeda.

"Tunadhani lazima kulikuwa na aina fulani ya mtandao uliomsaidia bin Laden nchini Pakistan, lakini hatufahamu nani aliyemsaidia wala mtandao huo ni upi. Hatujui kama ni watu walio ndani ama nje ya serikali, na hilo ni jambo ambalo tunapaswa kulichunguza na muhimu zaidi ambalo serikali ya Pakistan inatakiwa kulichunuza."

Mahojiano ya rais Obama na televisheni ya CBS yalikuwa ya kwanza marefu kuyafanya na kituo hicho, tangu kikosi maalumu cha wanajeshi wa Marekani kilipofanya oparesheni ya kumuua Osama bin Laden wiki moja iliyopita. Katika mahojiano hayo Obama anakiri kwamba zilikuwa dakika 40 ngumu zaidi katika maisha yake akisema hali ilikuwa ya wasiwasi mkubwa.

Flash-Galerie Bin Laden Verfolgung Verfolgungsjagd Versteck USA
Makazi ya Osama, kijiji cha Thanda Choha, Abottabad.Picha: picture-alliance/dpa

Obama ameitaka serikali ya Pakistan ichunguze nani aliyemsadia Osama. Mshauri wa masuala ya usalama wa rais Obama, Tom Dinilon, ameiambia televisheni ya Marekani ya NBC kwamba mpaka sasa hakuna ushahidi kwamba serikali, jeshi wala idara ya ujasusi ya Pakistan ilijua kwamba Osama bin Laden alikuwa akiishi nje kidogo ya mji mkuu Islamabad. Mshauri huyo ameitaka serikali ya Pakistan itoe taarifa kwa Marekani kuhusu Osama ilizopata kutoka kwa makazi yake na pia Marekani iweze kuwafikia wake watatu wa Osama, walio mikononi mwa vyombo vya usalama vya Pakistan.

Serikali ya Marekani inaongeza shinikizo dhidi ya Pakistan, lakini wakati huo huo inapongeza ushirikiano uliopo kufikia sasa. Obama amesema hakuna mahala popote ambako magaidi wengi wameuwawa kama nchini Pakistan, na hayo yote yamewezekana kupitia msaada wa viongozi wa nchi hiyo.

Mbali na jukumu la serikali ya Pakistan kutofahamika wazi, kwa upande mwingine kuna mjadala unaopamba moto katika bunge la Marekani, wa kutaka msaada wa mabilioni ya fedha kwa ajili ya Pakistan upunguzwe. "Kabla kuendelea kutuma fedha Pakistan lazima tuwe na uhakika kuwa Pakistan iko upande wetu katika vita dhidi ya ugaidi," amesema seneta Frank Lautenberg, wa chama cha Democratic. Naye seneta John Kery kwa upande wake ameiambia televisheni ya CBS kuwa anaona fursa kubwa ya kutathmini upya uhusiano kati ya Marekani na Afghanistan na Pakistan.

Mwandishi: Markwald, Nicole/Washington (HR)

Tafsiri:Nyiro Charo, Josephat

Mhariri: Saumu Mwasimba