1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama aendelea na ziara yake China

Kabogo Grace Patricia16 Novemba 2009

Kesho Jumanne Rais Obama atakutana na Rais Hu Jintao

https://p.dw.com/p/KY3w
Rais Barack Obama wa Marekani akiwa na Rais Hu Jintao wa China, mjini New York, Sept. 22, 2009.Picha: AP

Rais Obama ambaye yuko katika ziara yake ya kwanza nchini China amesema China na Marekani zinahitaji kuwa na uhusiano mzuri usiokuwa wa kiadui. Akiwahutubia wanafunzi katika ukumbi wa makumbusho ya sayansi na teknolojia mjini Shanghai, Rais huyo wa Marekani ametoa wito wa kuwepo kwa majadiliano ya wazi baina ya mataifa hayo mawili.

Baada ya hotuba yake Rais Obama alijibu maswali ya kiasi wanafunzi 500 waliochaguliwa, ambapo maswali mengi waliyouliza yalikuwa kwa njia ya mtandao wa Internet. Rais Obama alisema anataka majadiliano ya wazi baina ya nchi hizo mbili na kuzungumzia kuhusu ushirikiano wa karibu hasa katika sekta ya biashara, nishati na masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa eneo hilo, udhibiti wa silaha na sayansi.

Uhuru wa kujieleza na kuabudu

Rais Obama pia amezungumzia suala la udhibiti, akisema kuwa ukosoaji wa viongozi wa kisiasa lazima uruhusiwe na upatikanaji huru wa habari katika mtandao wa Internet lazima uzingatiwe. Rais huyo wa Marekani amesema uhuru wa kujieleza na kuabudu, upatikanaji wa habari lazima vipatikane kwa watu wote. Rais Obama alisema:

''Hatutaki kuweka mfumo wowote wa serikali kwa taifa jingine lolote, lakini pia hatuamini masuala muhimu tunayoyaunga mkono ni ya kipekee kwa taifa letu. Uhuru wa kujieleza na kuabudu, uhuru wa upatikanaji wa habari na ushiriki katika siasa tunaamini ni haki za msingi kwa watu wote. Lazima vipatikane kwa watu wote wakiwemo wale wa kutoka makabila na dini chache hata kama wako Marekani, China au katika taifa lolote lile.''

Rais Obama amesema matatizo makubwa hayawezi kutatuliwa hadi hapo nchi kubwa na yenye nguvu duniani pamoja na nchi inayoibukia katika ushindani zifanye kazi kwa kushirikiana pamoja.

Yatakayozungumzwa kesho Jumanne

Tayari Rais Obama amewasili mjini Beijing ambako kesho Jumanne atafanya mazungumzo na Rais Hu Jintao wa China pamoja na viongozi wengine wa kisiasa wa nchi hiyo. Aidha, Rais Obama amesema masuala yote yaliyotajwa katika hotuba yake mjini Shanghai yatajadiliwa katika mazungumzo yake na Rais Hu. Mada zinazotazamiwa kujadiliwa katika mkutano wa viongozi hao wawili ni pamoja na masuala ya kibiashara, mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na suala la nyuklia katika nchi za Korea Kaskazini na Iran pamoja na vita nchini Afghanistan na Pakistan. Mbali na masuala hayo Rais Obama atazungumzia pia suala la haki za binaadamu nchini China, wakati makundi ya kutetea haki za binaadamu yakisema polisi wamewakamata wanaharakati kadhaa mjini Beijing na maeneo mengine ya nchi hiyo. Kundi la CHRD limesema viongozi wa China walihofu kuwa wanaharakati hao ambao ni wakosoaji wangekutana na Rais Obama, maafisa wa Marekani au waandishi habari wa kigeni wanaoripoti ziara ya kiongozi huyo wa Marekani nchini China.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/APE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman