1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais na Wabunge wapigiwa kura Sierra Leone

P.Martin10 Agosti 2007

Chaguzi za rais na bunge zinazofanywa hii leo nchini Sierra Leone zinatazamwa kama ni mtihani muhimu kwa demokrasia katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/CH9l
Rais Ahmad Tejan Kabbah wa Sierra Leone hatogombea urais
Rais Ahmad Tejan Kabbah wa Sierra Leone hatogombea uraisPicha: AP

Hii ni mara ya pili kwa Sierra Leone kuwa na uchaguzi,tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa katili kabisa katika historia ya kisasa.Kiasi ya Wasierra Leone milioni 2.6 wana haki ya kuwachagua wagombea uchaguzi kutoka vyama saba vya kisiasa.

Lakini mchuano halisi,ni kati ya vyama vikuu viwili vilivyotawala nchini humo kwa muda mrefu, tangu taifa hilo kupata uhuru wake kutoka Uingereza katika mwaka 1961.

Rais Ahmad Tejan Kabbah,alieingia madarakani mwaka 1996 na kuchaguliwa tena mwaka 2002 amemteua Naibu rais Solomon Berewa kama mrithi wake.Uchaguzi wa rais unatazamiwa kuwa mchuano mkali kati ya Berewa alie na miaka 69 na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha APC,Ernest Koroma mwenye miaka 53;na viongozi hao wawili huenda wakalazimika kupambana tena katika duru ya pili.

Kwa upande mwingine,wagombea 566 wanapigania kuingia katika bunge lenye viti 112.Katika bunge hilo pia kuna machifu wakuu wa kitamaduni wapatao 12.

Lakini ni uchaguzi wa rais hasa unaongojewa kwa hamu kubwa,kwani kwa mujibu wa katiba ya nchi, Rais Kabbah haruhusiwi kugombea awamu nyingine. Kwa hivyo,wananchi wanatumaini kuwa mrithi wa Kabbah,atahifadhi amani na hatimae kutakuwepo masikilizano nchini humo,ambako uchumi umezorota vibaya.

Wananchi hawaridhiki na hali ya mambo na vijana ndio hawana matumaini.Kwa sababu hiyo,kura za waliokuwa watoto-wanajeshi,huenda zikawa muhimu kwa matokeo ya chaguzi za leo.Kwani ni rahisi kwa chama cha mgombea urais,Ernest Koroma kuwashawishi vijana hao.Chama cha Koroma cha APC kilichotawala Sierra Leone mpaka vita vya wenyewe kwa wenywe kuanza katika mwaka 1991,kimeungana na maadui wa zamani waliokuwa waasi wa kundi la RUF. Kundi hilo lilitawala kwa kusaidiwa na aliekuwa rais wa Liberia,Charles Taylor,kwa pesa zilizotokana na biashara ya almasi.

Suala jingine muhimu,linahusika na Mahakama Maalum ya Umoja wa Mataifa ya Sierra Leone.Hivi sasa,tena kunafanywa matayarisho ya kuendelea na kesi ya mshtakiwa mkuu,Charles Taylor.Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu,Stephen Rapp,sasa ni wakati muhimu wa kuendelea na kesi ya Taylor, inayosikilizwa mjini Den Haag nchini Uholanzi kwa sababu za usalama.

Inatathminiwa kuwa wakati wa vita vya Sierra Leone,kati ya mwaka 1991 na 2001,kiasi ya watu 120,000 waliuawa na maelfu wengine walikatwa viuongo na kubakwa.Maelfu ya raia hao waliteswa na waasi wa kundi la RUF.

Baada ya Slobodan Milosevic aliekuwa rais wa Yugoslavia ya zamani,Taylor ni kiongozi wa pili wa zamani kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.