Rais Mugabe wa Zimbabwe kugombea duru ya pili ya uchaguzi
5 Aprili 2008Tangazo hilo linadhihirisha kuwa chama tawala kinakiri hadharani kuwa Mugabe anaetawala tangu miaka 28 iliyopita hakufanikiwa kumshinda kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC katika duru ya kwanza.Matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais uliofanywa tangu Jumamosi iliyopita yangali yakingojewa.
Kwa upande mwingine,mgogoro mpya umezuka kuhusu matokeo ya uchaguzi wa bunge ambao pia ulifanywa Jumamosi iliyopita.Ingawa chama cha MDC kilitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe kama mshindi wa uchaguzi wa bunge, chama cha Mugabe ZANU-PF kinapinga matokeo hayo.Chama cha Mugabe kinachotawala tangu miaka 28 iliyopita, kinataka kura zihesabiwe upya katika wilaya 16.
Wakati huo huo chama cha MDC kimedai kuwa Morgan Tsvangirai amemshinda Mugabe katika uchaguzi wa rais.Hii leo mawakili wa MDC wanakwenda mahakamani mjini Harare kwa azma ya kuwahimiza maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanywa tangu juma moja lililopita.
Zimbabwe ambayo hapo zamani ilikuwa ikiyalisha mataifa mengine barani Afrika,leo hii inaagizia chakula kutoka nje na hutegemea msaada kuwalisha wananchi wake.Uchumi wa nchi hiyo umeporomoka vibaya mno.Wazimbabwe wanapambana na ughali wa maisha uliopindukia asilimia 100,000 na idadi ya watu wasio na ajira ni zaidi ya asilimia 80.