Rais Mugabe azomewa bungeni
26 Agosti 2008Nchini Zimbabwe rais Robert Mugabe amelifungua bunge huku akizomewa na wabunge wa chama kikuu cha upinzani cha Movement For Demokratic Change MDC.Licha ya upinzani huo aliokabiliana nao rais Mugabe amesema bungeni kwamba kuna kila uwezekano wa kufikiwa makubaliano juu ya kugawana madaraka ili kuumaliza mgogoro wa kisiasa ulioibuka kufuatia uchaguzi wa rais.
Rais Robert Mugabe alijizatiti kupaza sauti ili hotuba yake isikike bungeni lakini ikamezwa na makelele ya wabunge wa chama cha upinzani waliokaa katika viti vya upande wa chama tawala kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 28.
Wabunge hao wa upinzani ambao mwanzoni walitishia kususia ufunguzi rasmi wa bunge wakisema hawamtambui Mugabe kama rais wa taifa hilo walisikika bungeni wakisema chama cha ZANU PF kimeoza.
Chama cha MDC kilibadilisha msimamo wake baada ya mgombea wake wa nafasi ya Spika wa Bunge Lovemore Moyo kushinda hapo jana dhidi ya mgombea wa chama cha Zanu Pf.
Spika Moyo ambaye awali alionekana kutokubaliana na wazo la kumpokea rais Muga Mugabe kuja kufungua bunge hilo akisema msimamo wa chama chake ni kwamba Zimbabwe haina rais kwa sasa pia alikuweko bungeni hii leo kumpokea rais huyo mwenye umri wa miaka 84 alipowasili katika sherehe hiyo ya ufunguzi wa kikao cha kwanza cha bunge.
Wakati akilihutubia bunge hilo juu ya kurudi kwake tena madarakani Mugabe alisema ushindi wake ulitawaliwa na visa vya kujutia na ghasia za kisiasa za hapa na pale lakini matamshi hayo yalizomewa kwa sauti kubwa na wabunge wa chama cha MDC wanaosema zaidi ya wanachama wake 125 waliuwawa na vijana wa rais Mugabe tangu mwezi wa Marchi.
Aidha wabunge hao wenye hasira walizidi kumzomea rais aliposema kwamba makubaliano ya kihistoria yamekwisha kamilika na kila upande unatarajiwa kuridhika na kutia saini makubaliano hayo.
Mazungumzo kati ya ZANU PF na MDC yamekwama juu ya kile upinzani unachosema ni kukataa kwa Mugabe kuachilia madaraka makubwa ya urais baada ya kutawala kwa kipindi cha miaka 28.
Kwa upande mwingine rais Mugabe amekuwa akimtaja mara kwa mara Kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kuwa muharibifu kwa kushindwa kukubaliana na matakwa yakekuhusu kugawana madaraka ambapo anataka asalie na madaraka makubwa na Tsangirai achukue wadhifa wa waziri mkuu usiokuwa na usemi wowote.
Na kama kawaida yake hakukosa kuwashutumu wamagharibi rais Mugabe amesema hali mbaya ya uchumi iliyochangia mfumko mkubwa wa bei pamoja na ukosefu wa usalama ni kazi ya mikono ya waharibifu wakubwa na maadui wa nje.
Hata hivyo kipingamizi kikubwa hivi sasa kitakachomkabili rais Mugabe ni suala la kuliteuwa baraza jipya la mawaziri hasa ikizingatiwa ushindi wa upinzani katika nyadhifa za spika wabunge na kiongozi wa bunge la seneta.
Wakati huohuo polisi wanaendelea na kamatakamata dhidi ya wanachama wa MDC ambapo leo wamemtia nguvuni Elton Mangoma mmojawapo wa wajumbe katika mazungmzo ya upatanishi na chama cha ZANU PF.
►◄