1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mstaafu wa Cape Verde Pires atangazwa mshindi wa Tuzo ya Mo Ibrahim .

Abdu Said Mtullya10 Oktoba 2011

Pedro Pires wa Cape Verde ndiye Mshindi wa Tuzo ya Mo Ibrahim safari hii.

https://p.dw.com/p/12pCz
Rais Mstaafu wa Cape Verde Pedro Pires.Picha: AP

Kamati ya Mo Ibrahim imesema mjini London kuwa imemtangaza Bwana Pedro Rodriguez Pires kuwa mshindi wa tuzo ya utawala bora ,kutokana na mafanikio yake katika kuleta demokrasia,uimara na neema katika kisiwa cha Cape Verde. Kamati hiyo imesema katika tangazo lake leo mjini London kwamba, katika uongozi wake wa miaka 10 katika kisiwa cha Rasi ya Verde, kwenye pwani ya magharibi mwa Afrika ,Pedro Verona Pires aliweka msingi wa kuwaondoa wananchi wake 200,000 kutoka kwenye umasikini. Kutokana na utawala wake bora Pires alitambulika duniani kwa sera zake za kutekeleza haki za binadamu.

Wanakamati wa Mo Ibrahim wametilia maanani kwamba Rais Mstaafu Pedro Rodriguez Pires alilikataa wazo la kuibadilisha katiba ili kumwezesha kugombea Urais tena. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 77 aliutumia muda wa miaka 50 wa maisha yake katika shughuli za kisiasa.

Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mnamo mwaka wa 1975 na aliutumikia wadhifa huo kwa muda wa miaka 16 kabla ya kuwa Rais. Baadae alishindwa katika uchaguzi uliofanyika kwa mara ya kwanza katika kisiwa chake cha Cape Verde kwa njia za kidemokrasia mnamo mwaka wa 1991. Lakini alichaguliwa tena mnamo mwaka wa 2001 kwa kipindi cha miaka mitano, kilichofuatiwa na kingine mnamo mwaka wa 2006.

Rais Mstaafu Pedro Rodriguez Pires aliuweka msingi uliokigeuza kisiwa chake cha Cape Verde kuwa mfano wa demokrasia,uimara wa kisiasa na neema.

Katika maelezo yaliyotolewa mjini London na Kamati ya Mo Ibrahim wanakamati wametilia maanani kwamba kisiwa cha Rasi ya Verde ni mfano wa mafanikio ya kiuchumi, kijamii na kisiasa barani Afrika.

Pedro aliyatetea maadili ya ubinadamu kama alivyosema baada ya kutangazwa mshindi wa Tuzo ya Mo Ibrahim. Bwana Pedro Rodriguez Pires amesema katika harakati zake za kisiasa alikuwa na kaulimbiu ya maneno matatu- Kazi,Ukweli na Utiifu"

Alizaliwa mnamo mwaka wa 1934 katika kisiwa cha Cape Verde na alisoma kwenye shule ya msingi na ya upili katika kisiwa hicho kabla ya kuenda kwenye Chuo Kikuu cha Lisbon nchini Ureno mnamo mwaka 1956. Lakini kabla ya kuhitimu shahada yake , aliitwa ili kulitimikia jeshi la Ureno kama afisa wa kikosi cha anga.

Lakini mnamo mwaka wa 1961 pamoja na vijana wengine wa Kiafrika aliondoka Ureno kimya kimya,na kujiunga na chama cha ukombozi wa Guinea na Cape Verde, PAIGC kilichokuwa kinaongozwa na Amilcar Cabral mpigania uhuru jarabati.

Alifanya bidii ya kuwahamisha vijana wa nchi yake kwa ajili ya harakati za ukombozi . Mnamo mwaka wa 1974 Pires aliuongoza ujumbe wa chama chake cha PAIGC kwenye mazungumzo na serikali ya Ureno juu ya kuleta uhuru wa Cape Verde. Na tarehe 5 ya mwezi wa Julai mwaka 1975 Cape Verde alitangaza uhuru wake.

Mwandishi/Marta Barroso/

Tafsiri /Mtullya Abdu/

Mhariri/Josephat Charo/