Rais mpya wa Ufaransa anatazamiwa kuwasili Berlin
16 Mei 2007Rais mpya wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anatazamiwa kuwasili Berlin, hivi punde.Ziara hii imesadif muda mfupi tuu baada ya kukabidhiwa hatamu za uongozi nchini mwake.
Nicolas Sarkozy amekua rais wa sita wa jamhuri ya tano ya Ufaransa hii leo na kuahidi kufanya kila liwezekanalo kutowavunja moyo wafaransa.Rais Sarkozy amesema atatanguliza mbele “ bidii na ujuzi bila ya kutilia maanani ni kutoka chama gani.
“Nnatilia maanani kwa dhati jukumu walilonikabidhi wafaransa na nnaahidi sitowavunja moyo”amesema rais Sarkozy akisisitiza
“Nitakua rais wa jamhuri ya wafaransa wote bila ya kumtenga yoyote.”
Baada ya kuhutubia taifa ,kiongozi huyo mpya wa Ufaransa akiongozana na askari waliopanda mapikipiki na walinzi wa jamhuri,aliutembelea uwanja mashuhuri wa Champs Elysée,akiwapungia mkono na akuwashukuru mamia ya watu waliokua wakimshangiria.
Baadae aliweka shada la mauwa katika sanamu la George Clémenceau kabla ya kuupiga mguu hadi mahala lilikowekwa sanamu la General Charles De Gaule na kuweka pia shada la mauwa.
Baadae leo jioni rais Nicolas Sarkozy anatazamiwa kuelekea Berlin kwa mazungumzo pamoja na kansela Angela Merkel mwenyekiti wa sasa wa umoja wa ulaya.
Kwa kufanya ziara yake ya kwanza rasmi nchini Ujerumani,tena mara tuu baada ya kuapishwa,rais Nicolas Sarkozy ameonyesha azma yake ya kutaka kusaidia kuukwamua umoja huo unaokumbwa na mzozo tangu katiba yake ilipokataliwa nchini Ufaransa na Uholanzi pia.
Rais Nicolas Sarkozy atapokelewa kwa hishma za kijeshi na kansela Angela Merkel kabla ya kukutana na waandishi wa habari na baadae kujitenga kwaajili ya mazungumzo ya ana kwa ana.
Wadadisi wameshaanza kujiuliza Nicolas Sarkozy ataendeleza na yeye pia desturi za mtangulizi wake Jacques Chirac anapoonana na kansela Angela Merkel?”Kila atakachofanya,kila atakalosema,kitapimwa na kuchujwa katika kutathmini uhusiano uliokuwepo kati ya Ufaransa na Ujerumani na jinsi utakavyokua baada ya kuingia madarakani Nicolas Sarkozy.
Miongoni mwa mada ambazo kansela Angela Merkel anapanga kuzungumzia pamoja na rais mpya wa Ufaransa ni pamoja na mkutano wa kilele wa mataifa manane tajiri kwa viwanda,june tano had nane ijayo,mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya june 21 na 22 ijayo na azma ya Ujerumani ya kusaka ridhaa ya mataifa 27 wanachama wa umoja wa ulaya kuhusu namna ya kubuniwa katiba mpya ya Umoja wa ulaya.
Hali ya kimataifa na hasa mivutano ya hivi karibuni kati ya Umoja wa ulaya na Urusi ni miongoni mwa mada zitakazojadiliwa mjini Berlin kati ya kansela Angela Merkel na rais Nicolas Sarkozy .
Kansela Angela Merkel angependelea kumuona rais
Sarkozy akiwajibika zaidi kwaajili ya Umoja wa Ulaya.
Magazeti ya Ujerumani yameshangazwa na jinsi Nicolas Sarkozy alivyoharakisha kutia njiani marekebisho katika shughuli za uongozi katika kasri la Elysée.“Nicolas Sarkozy anarekebisha mambo kwa haraka kupita kiasi na kujiimarishia madaraka“ limeandika gazeti la mrengo wa kati kushoto SÜDDEUTSCHE ZEITUNG huku gazeti la kihafidhina la Die WELT likizungumzia kiu cha kutaka makubwa,kama alivyokua Napoleon.