Rais Morales wa Bolivia ajiuzulu
11 Novemba 2019"Ni mapinduzi kwasababu jeshi lilimtaka rais ajiuzulu jambo linalokwenda kinyume cha katiba ya nchi hiyo," alisema Erbrad.
Rais Morales alijiuzulu kufuatia shinikizo kutoka jeshi la nchi hiyo, baada ya shutuma kwamba ushindi wake katika uchaguzi uliopita ulipatikana kwa njia za ulaghai. Kiongozi huyo amekuwa akikabiliwa na maandamano ya umma, na ukosoaji kutoka jumuiya ya kikanda.
Uamuzi huo wa Rais Evo Morales unajiri baada ya siku iliyokuwa na matukio mengi ikiwa ni pamoja na pendekezo alilolitoa awali la kuandaliwa kwa uchaguzi mpya. Mzozo huo uliendelea kuwa mbaya zaidi wakati mkuu wa majeshi alipozungumza kupiti runinga ya taifa, akimtaka wazi wazi Rais Morales kuondoka. Katika tangazo la kujiuzulu, Morales ambaye ni mfuasi wa siasa za kisoshalisti amesema amefanya hivyo baada ya kushauriana na washirika wake.
Morales mwenyewe anasema kuondoka kwake ni kutokana na mapinduzi
"Kwa kaka na dada zangu wa Bolivia na ulimwengu mzima, nataka kuwafahamisha kuwa niko hapa na naibu rais na waziri wa Afya, na kwamba baada ya kuwasilikiliza rafiki zangu kutoka shirikisho la vuguvugu la kijamii na shirikisho la umoja wa kibiashara na pia kwa kusikiliza kanisa katoliki, natangaza kujiuzulu wadhifa wangu wa urais," alisema Morales.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 60, aliongeza kuwa kuondoka kwake ni kutokana na ''harakati za mapinduzi''. Hata kabla ya Morales kumaliza taarifa yake, watu walianza kushangilia huku wakipiga honi za magari mjini La Paz na miji mingine na kuenda barabarani kusherehekea huku wakipeperusha bendera za nchi hiyo na kuwasha baruti.
Makundi makubwa ya watu yalikusanyika katika maeneo ya mji huo mkuu huku wengi wakisherehekea na wengine wakibubujikwa na machozi ya furaha . Waandamanaji walijilaza mbele ya ikulu ya rais na kuteketeza jeneza kuashiria kifo cha serikali ya Morales.
Hata hivyo haikubainika wazi nani atakayemrithi Morales.
Kutokana na hatua hiyo ya kujiuzulu kwa rais huyo wa Bolivia, mshirika wake katika ukanda wa Amerika Kusini, rais wa Venezuela Nicolas Maduro amesema kuwa atasimama naye na kudai kwamba Morales amekuwa mhanga wa njama inayoungwa mkono na Marekani inayotaka kumng'atua mamlakani na kumuweka kiongozi anayeegemea siasa za mrengo wa kulia.
Mexico itatoa hifadhi kwa Morales
Maduro na Morales wanaoegemea sera za mrengo wa kushoto ni marafiki wa kisiasa wa muda mrefu.
Wakati huo huo, viongozi wa chama cha kisosiolisti nchini Venezuela wametoa wito kwa raia wa Venezuela kujiunga na maandamano Jumamosi ijayo kuonyesha umoja wao na Morales.
Huku hayo yakijiri, waziri wa mambo ya nje wa Mexico Marcelo Ebrard amesema jana kuwa nchi yake itatoa hifadhi kwa Morales iwapo atataka kuchukuwa hatua hiyo katika ishara mpya ya Mexico ya kujihusisha na serikali zinazoegemea siasa za mrengo wa kushoto katika Amerika Kusini.
Ikiongozwa na rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador, serikali ya nchi hiyo ilitoa ujumbe mkali wa kumtetea Morales.
Morales ni mtu wa kwanza kutoka jamii asilia ya Bolivia kuwa rais na amekuwa mamlakani kwa takriban miaka 13.