1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Magufuli awaonya wenye vyeti bandia Tanzania

1 Mei 2017

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewapa siku kumi na tano wafanyakazi zaidi ya elfu kumi waliobainika kughushi vyeti na kujipatia ajira katika serikali kujiondoa haraka kabla ya mkono wa sheria kuwafikia

https://p.dw.com/p/2cC22
Tansania Afrika  John Pombe Magufuli
Picha: DW/C.Ngereza

Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika hotuba yake katika kilele ya siku ya wafanyakazi duniani iliyoadhimishwa kitaifa nchini Tanzania Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro. Magufuli amesema kuwa wafanyakazi hao walioghushi vyeti wameisababaishia serikali kupoteza mabilioni ya shilingi na kufanya kazi chini ya viwango kutokana na wengi kutokuwa na taaluma ya majukumu waliyo nayo.

Katika hatua nyingine rais Magufuli ametaja kundi lingine la watu ambao amesema wamepunguza tarakimu za umri wao ili kuendelea kubaki kazini wanachunguzwa na wakibainika hatua za kisheria zitachukua mkondo.

Rais Magufuli ambaye alichukua muda mrefu kuelezea changamoto za serikali yake amesema wafanyakazi nchini Tanzania wataneemeka baada ya serikali yake kurekebisha mambo ambayo yamekuwa yakisababisha fedha kupotea kwa njia za kijinai.

Mara baada ya rais kutangaza mikakati ya kukabili wafanyakazi waliogushi vyeti na wanaoongeza umri waendelee kubaki kazini baadhi ya wafanyakazi walionekana kuridhika na jitihada za rais na kutaka watu hao kuchukuliwa hatua haraka.

Awali shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi nchini Tanzania kupitia katibu wake Dr.Yahaya Msigwa lilimwomba rais Magufuli kuongeza kiwango cha kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi laki moja na nusu hadi laki saba na nusu akidai ndio kiwango kinachoweza kuwafanya wafanyakazi kumudu hali ya maisha. Aidha Dr.Msigwa katika risala yake kwa rais aliomba serikali kupunguza kiwango cha kodi zinazotozwa katika mishahara ya wafanyakazi katika ngazi za kati na juu badala ya sasa ambapo wanaofaidi afueni hiyo ni wafanykazi wa kada ya chini.

Shirikisho hilo pia lilizungumzia tatizo la kuchelewa kwa kesi za wafanyakazi wanaotafuta haki katika mahakama tatizo alilosema limekuwa sigu huku likiwapa wafanyakazi wanaotafuta haki mateso makubwa.

Hata hivyo rais Magufuli ambaye  katika sherehe hizo aliongozana na serikali yake yote akiwemo Makamu wa rais bibi Samia Suluhu Hassan ,waziri mkuu Kassim Majaliwa, spika wa bunge Job Ndugai, katibu kiongozi John Kijazi pamoja na mawaziri kadhaa, aliwahakikishia wafanyakazi kuwa mara serikali itakapomaliza kushughulikia matatizo ya wafanyakazi hewa na waliogushi vyeti itawaongezea mishahara katika bajeti ijayo.

Mwandishi: Charles Ngereza
Mhariri: Iddi Ssessanga