1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Magufuli atangaza siku 7 za maombolezo ya Mkapa

24 Julai 2020

Rais wa Tanzania John Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo na bendera kupepea nusu mlingoti, kufuatia kifo cha aliekuwa rais wa awamu ya tatu wa taifa hilo Benjamini William Mkapa.

https://p.dw.com/p/3frYe
Tansania Ex-Präsident Benjamin Mkapa gestorben
Picha: DW/Said Khamis

Akitangaza kutokea kwa msiba huo rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania John Magufuli amesema, Rais huyo mstaafu amefariki wakati akipokea matibabu hospitalini mjini Dar es salaam, hivyo taifa litasalia kwenye maombolezo kwa muda wa siku saba.

Marehemu Mkapa alieingia mamlakani mwaka 1995 akichaguliwa katika uchaguzi wa kwanza uliotawaliwa na siasa za ushindani akiongozwa na falsafa ya uwazi na ukweli aliliongoza taifa huku akiipa kipaumbele sekta binafsi anatajwa kukumbukwa katika masuala ya upatanishi kwa nchi za afrika pale zilipotumbukia katika migogoro ya ndani na ile ya nchi na nchi.

Rais Magufuli (kushoto) akisalimiana na Benjamin Mkapa (kulia) 04.11.2018
Rais Magufuli (kushoto) akisalimiana na Benjamin Mkapa (kulia) 04.11.2018Picha: DW/Said Khamis

Mashirika ya kiraia nchini Tanzania yanautaja msiba huo kuwa ni pigo kwa bara la Afrika kutokana na kiongozi huyo kuwa mstari wa mbele katika kuleta upatanishi katika migogoro iliyoshuhudiwa katika mataifa kadhaa barani humo, kadhalika hakusita kukemea hadharani uongozi uliotajwa kuwa dhalimu na kunyonya watu wake, huku akisisitiza kuwekeza kwa vijana ili kuwa na viongozi wenye uzalendo hapo baadae.

Kitaaluma Mkapa alikuwa ni mwanahabari, ambae hadi sasa ameandika kitabu chake kinachosomeka kwa kimombo my life my purpose kikielezea maisha yake na hata awamu yake ya uongozi, huku akikiri kuwa na mapungufu katika baadhi ya maamuzi, hivyo kuwataka viongozi wajao kuchukua kama funzo. 

Watanzania watoa hisia mbalimbali kumuomboleza Mkapa

Bado taarifa zaidi hazijatangazwa na serikali ya tanzania kuhusiana na taratibu za mazishi za kiongozi huyo ambae amefariki akiwa na umri wa miaka themanini na mbili.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam