1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Magufuli aapa kuushinda nguvu Ufisadi

11 Desemba 2015

Tanzania na Juhudi za Rais mpya John Pombe Magufuli za kupiga vita rushwa na ,Mkutano wa sita wa kilele kati ya nchi za Afrika na China ni miongoni mwa mada za Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii

https://p.dw.com/p/1HLlo
Rais wa Tanzania akijiunga na mpango wa kusafisha nje ya ikulu ya rais jijini Dar es SalaamPicha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Tuanzie lakini Tanzania.Mnamo wiki hii ambapo walimwengu waliadhimisha siku ya kimataifa ya kupambana na rushwa-kauli mbiu mwaka huu ikiwa "Kata mnyonyoro wa ufisadi",magazeti ya Ujerumani yalielekeza dira zao katika nchi mbali mbali za Afrika Lilikuwa gazeti la kusini mwa Ujerumani "Süddeutsche Zeitung" lililochambua juhudi za kupambana na rushwa za rais mpya wa Tanzania John Pombe Magufuli."Tingatinga" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya Süddeutsche,likifuata jina la utani la rais mpya wa Tanzania kutokana na juhudi zake za kupambana na rushwa nchini humo.Baada ya kuelezea namna zoezi la uchaguzi lilivyopita na kusema lilikuwa nusra lizushe mageuzi,ya kwanza ya kidemokrasia katika historia ya nchi hiyo,Süddeutsche Zeitung linaandika"kwa mara nyengine aliyeshinda katika uchaguzi huo mwishoni mwa mwezi wa octoba alikuwa mgombea wa chama tawala CCM"."Waliofikiri mambo yangeendelea kama ilivyokuwa wamekosea." Kwasababu kwa kuchaguliwa Magufuli kuwa rais mpya wa Tanzania,yamezuka maajabu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki,licha ya chama tawala. Süddeutsche Zeitung linaelezea jinsi rais John Pombe Magufuli alivyoitembelea wizara ya fedha bila ya kutoa taarifa mara baada ya kuchaguliwa,jinsi alivyotangaza marufuku kwa maafisa wa ngazi ya juu serikali kutembelea nchi za nje-pesa hizo kutakiwa ziwekezwe kwengineko-kwa mfano elimu kuanzia mwakani itakuwa bure mpaka katika shule za sekondari. Jinsi Magufuli alivyoitembelea ghafla hospitali kuu na kumwachisha kazi mkuu wa hospitali pmoja na kulivunja baraza la usimamizi.Na mnamo siku ya 19,linaandika Süddeutsche,rais John Pombe Magufuli akaamuru sherehe za uhuru zisisherehekewe. Badala yake fedha zitumike kupambana na maradhi ya kipindu pindu yaliyouwa dazeni kadhaa ya watu miezi iliyopita magharibi ya Tanzania. Badala ya sherehe,watanzania walitakiwa washiriki katika mpango wa kusafisha mitaa yao. Na siku ya 22,ikafuata ziara ya ghafla ya waziri mkuu wa Magufuli,Majaliwa Kassim katika bandari kubwa ya nchini hiyo jijini Dar es Salaam.Watu waliposhindwa kumueleza ushuru wa makontena 350 umeishia wapi,Magufuli akamsitisha kazi kiongozi wa idara ya kodi ya mapato pamoja na maafisa wake watano wa ngazi ya juu.

Rais Magufuli yu madarakani kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche na kuongeza "kila kitu kinaonyesha kuwa,jina la "Tingatinga"hakupewa bure.

Nyota Nyekundu katika Anga ya Afrika

Mada nyengine ya Afrika iliyohanikiza katika magazeti ya Ujerumani wiki hii ni kuhusu mkutano wa 6 wa kilele kati ya jamhuri ya Umma wa China na Afrika mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini."Nyota nyekundu katika anga ya Afrika" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Berlin,die Tageszeitung" linaloelezea jinsi viongozi wa pande hizo mbili wanavyozungumzia kuhusu ushirikiano na uhusiano imara-lakini ukweli linasema ni mwengine kabisa. Kila mara husisitizwa katika mikutano ya kilele kama huu kwamba Afrika na China ndio matumaini ya karne ya 21-lakini mkutano wa mwaka huu wa kilele haukusimama katika nyota njema. China inanua idadi ndogo ya mali ghafi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma na bei katika masoko ya dunia imepungua kwa zaidi ya nusu. Mnamo miezi 12 iliyopita hadi kufikia october mwaka huu,bidhaa zinazoagiziwa na China zimepungua kwa asili mia 12 na kutoka Afrika kwa asili mia 30. Kutokana na hali hiyo nchi nyingi za Afrika zinazotegemea mapato ya biashara ya mafuta ghafi na maadini haziwezi tena kugharimia miradi ya uwekezaji na kupunguza nakisi ya bajeti.

Kinyume chake bidhaa za bei rahisi kutoka China zinazidi kuenea katika masoko ya Afrika. Katika wakati ambapo wezani wa kibiashara ulikuwa nusu kwa nusu kati ya pande hizo mbili hadi miaka miwili iliyopita,hivi sasa China ndio inayofadidika zaidi kwa biashara hiyo ikijipatia faida ya dala bilioni 40 kwa mwaka. Hali hiyo imegubika mkutano huu wa kilele mjini Johannesburg,linaandika die Tageszeitung linalomalizia kwa kuzungumzia azma ya China kutanguliza mbele hivi sasa miradi ya kueneza viwanda barani Afrika pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Basis/Presser/All/Presse

Mhariri: Iddi Ssessanga