Rais Macron aitisha mkutano wa dharura kufuatia ghasia
30 Juni 2023Ikulu ya Elysee imeeleza kuwa mkutano huo ambao utaikutanisha timu maalum ya mawaziri wenye kushughulikia migogoro utafanyika kuanzia saa saba leo adhuhuri.
Macron mwenyewe anahudhuria mkutano mwengine wa kilele mjini Brussels wa Umoja wa Ulaya na anatarajiwa kuukatiza na kurudi nyumbani.
Ghasia zimezuka kwa siku ya tatu mfululizo katika mji mkuu wa Paris pamoja na miji mingine ya Ufaransa jana jioni zilizochochewa na kifo cha kijana mwenye umri wa miaka 17 wakati wa ukaguzi wa polisi wa trafiki.
Soma zaidi:Hali tete Ufaransa watu 150 wakamatwa usiku kucha
Kifo cha Nahel, kimefufua upya malalamiko ya muda mrefu kuhusu tabia ya polisi wa Ufaransa kulenga watu weusi na waarabu pamoja na jamii zinazoishi katika vitongoji vya watu wenye kipato cha chini.
Magari na mapipa ya taka yamechomwa moto huku maafisa wa polisi wakishambuliwa kwa fashi fashi. Katika patashika hizo, jumla ya watu 667 wamekamatwa na maafisa wa polisi 249 wamejeruhiwa. Takwimu hizo zimetolewa na waziri wa mambo ya ndani Gerald Darmanin.
Waziri wa uchukuzi Clement Beaune amesema, "Lakini tunataka kuwa wazi kabisa kwa kusema watu wanafaa kuheshimu sheria za nchi na kwamba vurugu zinapaswa kulaniwa."
Polisi watumwa katika miji mbalimbali kukabiliana na ghasia
Maafisa wa usalama wapatao 40,000 wamemwagwa katika kila pembe ya nchi hiyo jana jioni ili kuzima ghasia hizo, huku 5,000 kati yao wakishika doria mjini Paris.
Utawala wa mji huo mkuu umeitisha kikao cha dharura na kubuni timu maalum ya kukabiliana na ghasia hizo.
Katika mahojiano yake ya kwanza na vyombo vya Habari, mamake Nahel, Mounia, ameliambia shirika la habari la France 5, "Siwalaumu polisi, bali namlaumu mtu mmoja tu, aliyemuua mwanangu.”
Ameongeza kuwa, afisa huyo wa polisi mwenye umri wa miaka 38, na ambaye alizuiliwa na kushtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, "aliona uso wa mwarabu, mtoto mdogo, na alitaka kumuua.”
Hali ya vurumai imeshuhudiwa pia kwenye miji mingine ya Ufaransa kama vile Marseille, Lyon, Pau, Toulouse na Lille. Maandamano ya kulaani mauaji ya Nahel yamefanyika pia nchi jirani ya Ubelgiji ambako watu 30 wamekamatwa kwa kufanya vurugu.
Soma pia:Rais Macron wa Ufaransa afungua mkutano wa kilele wa ufadhili
Serikali inajaribu kila iwezavyo kuepusha kujirudia kwa ghasia kama zilizotokea mnamo mwaka 2005, na ambazo zilichochewa na vifo vya wavulana wawili wenye asili ya Afrika wakati wa msako wa polisi. Katika ghasia za mwaka huo, watu 6,000 walikamatwa.
Rais Emmanuel Macron ametoa wito wa utulivu na kueleza kuwa maandamano ya vurugu hayana uhalali wowote.
Ghasia hizo ni changamoto mpya kwa rais Macron, ambaye pia hivi karibuni utawala wake ulikabiliwa na maandamano makubwa yaliyochochewa na utata juu ya mageuzi ya umri wa kustaafu ambapo serikali ilitaka kuuongeza kutoka miaka 62 hadi miaka 64.