Rais Kenyatta na makamu wake kuongezwa mshahara
9 Mei 2019Itakumbukwa kuwa wawili hao walipunguziwa mshahara mwaka 2017 kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8. Wakati huo huo, wabunge nao wanapania kujiongezea hela za kufadhili afisi zao za mikoani ifikapo Julai mwaka huu, huku spika wa bunge la taifa akiunga mkono mapendekezo hayo.
Viongozi hao wawili wakuu wa serikali watapokea jumla ya shilingi milioni 38 za Kenya za marupurupu na mshahara kwa mwaka kuanzia mwezi Julai. Kiasi hicho cha fedha bado kiko chini ikilinganishwa na kabla walipopunguziwa mshahara mwaka 2017. Wizara ya fedha ina mpango wa kutenga nyongeza ya 3.9% ya malipo ya mshahara wa Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto.
Mshahara utakuwa shilingi milioni 38 za Kenya
Kulingana na nyaraka za wizara ya fedha ambayo DW imeziona, mishahara ya viongozi hao wawili wa serikali kwa pamoja itaongezeka kutokea shilingi milioni 36.6 hadi 38 kwa mwaka. Mwaka 2017. Rais Uhuru na naibu wake William Ruto walipunguziwa mishahara kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8 ili kupunguza mzigo wa mishahara ya viongozi.
Kwa mantiki hii, mshahara wa rais ulipunguzwa kutokea milioni 1.65 hadi 1.44 kwa mwezi na naibu wake kupunguzwa kutokea milioni 1.4 hadi 1.23.
Kwa upande mwengine, wabunge wanajipangia shilingi bilioni 7.9 kugharamia maandalizi ya afisi zao za mikoani, kadhalika malipo ya wasaidizi wao kuanzia Julai mwaka huu. Tume ya kuwaajiri wabunge, PSC, inasaka ridhaa ya watunga sheria kuiongeza bajeti yao ya operesheni kwa shilingi milioni 440. Kwa sasa wabunge wamtengewa shilingi bilioni 6.8.
Spika wa bunge la taifa aliye pia mwenyekiti wa tume ya PSC, Justin Muturi, anaunga mkono mapendekezo hayo. Wabunge 349 na maseneta 67 wakiwemo wabunge maalum wana uwezo wa kuajiri madereva na wasaidizi kwa gharama ya serikali. Kwa sasa bunge la taifa limetengewa shilingi bilioni 6.1 mahsusi kugharamia mahitaji ya afisi za mikoani, nalo baraza la Senate limetengewa shilingi bilioni 1.17.
Ifahamike wazi kuwa mfanyakazi wa mbunge anayelipwa hela nyingi zaidi anapokea shilingi alfu 65 na wa kima cha chini zaidi anapokea shilingi alfu 20. Hata hivyo, shilingi bilioni 3.07 pekee ndizo zilizotengewa miradi ya maendeleo kati ya hela hizo zinazotafutwa.
Tayari wabunge wanapewa mkopo wa gari usiotozwa kodi, hela ya usafiri, malipo ya uzeeni na kadhalika posho za kuhudhuria vikao vya kamati za bunge. Kimsingi kila mbunge anajikusanyia shilingi milioni nzima kila mwezi.