Kwenye taarifa ya kurasa nne kwa vyombo vya habari, Rais Kenyatta alisema kuwa uamuzi huo, unaonesha kuwa mahakama ya ICJ imekiuka dhima ya utendajikazi wake hivyo kuingilia uhuru na idhini ya mataifa katika mchakato wa kupatikana kwa haki katika mahakama za kimataifa.
Aidha alielezea kujitolea kwake kusuluhisha mzozo huo kwa njia nzuri na kuwaomba Wakenya kutulia, kwa sababu serikali yake inashughulikia mzozo huo.
Soma pia: ICJ yaiunga mkono Somalia katika mzozo na Kenya
Uamuzi huo huenda ukayumbisha mahusiano kati ya mataifa hayo ambayo yamekuwa yakizozana kuhusu mpaka huo kwa kipindi cha miaka saba sasa. Tangu mwanzo, Kenya ilikuwa imesema kuwa haitaridhia uamuzi huo na hata kujiondoa kwenye vikao vya mahakamani.
“Sisi kama taifa linalopenda amani, hatutakubali kuingiliwa ama kutishwa, hatutakubali hata inchi moja ya taifa letu iingie kwa mikono ya watu wengine. Tuko tayari kuilinda nchi yetu jinsi tulivyo tayari kulinda amani za nchi nyingine,” amesema Kenyatta.
Jopo la majaji wa Mahakama ya Haki ya Kimataifa, iliyoko Hague, Uholanzi ilisema kuwa Kenya ilishindwa kuthibitisha kuwa iliafikiana na Somalia kuhusu mpaka kati yao katika bahari ya Hindi.
Mahakama hiyo iliipa Somalia kipande kikubwa kilicho na gesi na mafuta. Uamuzi ambao Rais Kenyatta alisema kuwa ulishindwa kuzipa nafasi asasi za kikanda kuutatua mzozo huo.
Soma pia: Nini chanzo cha uhasama kati ya Kenya na Somalia?
Matamshi ya Rais Kenyatta yanajiri huku Kenya ikiwa mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hali ambayo huenda suala hilo likawasilishwa kwa baraza hilo.
Hata hivyo Rais Kenyatta amesema kuwa atazingatia kiapo alichoapa alipoapishwa mwaka 2013 cha kuilinda mipaka ya taifa la Kenya.
Mahakama hiyo ilipuuza mwafaka ulioafikiwa mwaka 1979 kuhusu mpaka huo kati ya Kenya na Somalia na badala yake ikaamua kuwa mpaka uliowekwa na wakoloni mwaka 1934 uzingatiwe. Rais wa Somalia Mohammed Farmajo ameupongeza uamuzi wa mahakama hiyo.
“Kwanza ningependa kumshukuru Allah ambaye ametupa ushindi huu wa kihistoria, baada ya mvutano wa muda mrefu na serikali ya shirikisho ya jamhuri ya Somalia, dhidi ya majaribu haramu ya serikali ya Kenya, kudai sehemu ya himaya yetu,” amesema Mohammed Farmajo.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Somalia na Kenya mashakani
Kenya, ambayo ilikabidhiwa kipande kidogo cha eneo linalozozaniwa kwenye uamuzi huo, ilishindwa kuthibitisha kuwa kulikuwepo na mpaka kati ya mataifa hayo.
Eneo linalozozaniwa ni kilomita laki moja za mraba, na linaaminika kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta, gesi na samaki. Kenya ni miongoni mwa mataifa yenye wanajeshi wengi walio kwenya kikosi cha muungano cha kudumisha usalama nchini Somalia.
Makundi ya kigaidi kama vile al-Shabaab na al-Qaeda yanaaminika kujificha nchini Somalia. Haijulikani sasa ni hatua ipi Kenya itachukua baada ya uamuzi huo wa mahakama.