1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kenyatta akutana na Waziri Mkuu wa Abiy Ahmed

9 Desemba 2020

Kenya na Ethiopia zimekubaliana kuimarisha biashara baina ili kuboresha uchumi wa mataifa hayo. Viongozi wa mataifa hayo walizungumza wakiwa katika mji wa mpakani wa Moyale katika hafla ya kuzindua kituo cha forodha.

https://p.dw.com/p/3mTow
Bildcombo I Abiy Ahmed und  Uhuru Kenyatta

Suala la kuboresha biashara baina ya Kenya na Ethiopia lilitawala katika hafla ya kufungua kituo cha forodha mjini Moyale, Rais Kenyatta akiwahimiza Wakenya kutumia mpaka huo katika kuimarisha biashara zao.

Kenyatta amesema kufunguliwa kwa kituo hicho cha forodha kwenye mpaka huo, kutasaidia ukuaji wa mji wa Moyale akiulinganisha na mji wa Dubai katika siku zijazo. Aidha Rais Kenyatta amesema kituo hicho kitatoa nafasi za ajira kwa vijanja kutoka mataifa ya Kenya na Ethiopia.

Rais huyo wa Kenya ametahadharisha iwapo kutakuwa na tishio la kiusalama kwenye mpaka huo, kutapelekea yanayokusudiwa yakakosa kuafikiwa, na ametumia jukwaa hilo kuwahimiza wananchi kuwasaidia maafisa wa polisi kutunza amani kwa kuwapa taarifa.

"Ni sharti tushirikiane kama majirani katika kupambana na wanaotishia usalama miongoni mwetu, na ambao pia wanatishia kupatikana kwa amani na utulivu baina yetu sisi kama Kenya na Ethiopia,” amesema Kenyatta.

Kauli ya rais Kenyatta imeungwa mkono na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy ambaye amewataka wananchi kutoka mataifa yote mawili kusaidia katika kupambana na wanaotishia usalama.

Wegweiser Autobahnschild Äthiopien
Alama ya barabarabi katika eneo la mpakani la Moyale EthiopiaPicha: DW

Abiy hakugusia hali tete ya usalama Tigray

Waziri huyo mkuu amelitaja kundi la waasi la OLF kutoka Ethiopia na lile la kigaidi la al-Shabaab kama yanayoendelea kuhujumu juhudi za amani katika eneo hilo.

"Amani ni msingi kwa kila tunachotaka kufanya ili kubadilisha maisha ya watu wetu.Ikiwa tunaweza kuwaondoa Alshabaab na OLF kutoka eneo hili,mtashuhudia namna hawa watu wanavyoweza kubadilishiwa maisha kama familia, mtu mmoja, au taifa,” amesisitiza Abiy.

Hata hivyo, waziri huyo mkuu amekwepa kulizungumzia hali tete ya kiusalama nchini mwake katika mkoa wa Tigray.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya waitaka Ethiopia irudishe mawasiliano Tigray

Ufunguzi wa kituo hicho cha Forodha mjini Moyale utasaidia kuunganisha mji wa Hawassa nchini Ethiopia hadi Moyale nchini Kenya.

Baada ya kukamilika kwa hafla hiyo, Abiy na mwenyeji wake Kenyatta walielekea katika jimbo la Lamu kukagua mradi wa barabara kutoka Lamu, kuelekea Sudan kusini kupitia Ethiopia liliopewa jina LAPSSET.

Abiy yuko nchini Kenya kwa ziara ya siku mbili