Rais Kenyatta 'aishambulia' idara ya mahakama
2 Septemba 2017Kauli hiyo ya Kenyatta inakuja siku moja tu baada ya Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi wa tarehe 8 Agosti, ambao ulikuwa umempa ushindi Kenyatta dhidi ya mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, na kisha mahakama hiyo kuamuru mwengine mpya ndani ya siku 60.
Odinga, ambaye ndiye aliyefungua kesi ya kuweka zuio la ushindi huo wa Kenyatta uliotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), alikuwa anahoji kwamba kulikuwa na ghiliba nyingi kwenye matokeo ya IEBC.
Baada ya ushindi huo wa Ijumaa, sasa Odinga anataka IEBC nzima ivunjwe, lakini kwenye hotuba yake ya leo, Kenyatta ameionya mahakama dhidi ya kuiingilia kati tume hiyo ya uchaguzi.
"Tutaipitia upya hii kitu. Kwa kweli tuna tatizo fulani," alisema akimaanisha idara ya mahakama.
"Nani kwani hasa alikuchaguweni? Ni nyinyi? Tuna tatizo la lazima tulirekebishe," alisema wakati akihutubia moja kwa moja kupitia televisheni akiwa Ikulu ya Nairobi, mara tu baada ya kukutana na magavana na wateule wengine wa chama chake cha Jubilee.
Kenyatta alirejelea pia ujumbe wake wa siku ya Ijumaa (Septemba 1) kwamba angeliuheshimu uamuzi huo wa Mahakama ya Juu, unaochukuliwa kama hatua kubwa kabisa kwenye mahakama barani Afrika, ambako kawaida serikali zilizo madarakani huwadhibiti majaji.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumamosi (Septemba 2), Kenyatta alisema: "Kwa sasa, tukutane kwenye kisanduku cha kura."
Aishambulia mahakama mara ya pili mfululizo
Hii ni mara ya pili tangu uamuzi huo wa mahakama, kwa Kenyatta kutoa kauli kali hadharani dhidi ya idara ya mahakama.
Hapo Ijumaa, akizungumza kwenye mkusanyiko wa wafuasi wake jijini Nairobi, Kenyatta aliikosoa mahakama kwa kudharau matakwa ya Wakenya na kuwaita majaji wa Mahakama ya Juu kuwa ni 'wakora'.
Wachambuzi wanasema kauli hizi za sasa za Kenyatta dhidi ya idara huru ya mahakama zinaogofya sana.
"Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba Kenyatta anaonekana kutoa kauli za vitisho dhidi ya idara ya mahakama," alisema Murithi Mutifa, mchambuzi wa masuala ya Afrika katika Taasisi ya International Crisis ya Nairobi.
"Huu ulikuwa ni muda wa fahari kubwa kwa demokrasia ya Kenya, ambapo mahakama imeusimamisha utawala wa sheria. Wanasiasa wanapaswa kuchukuwa tahadhari ya kutowachochea wananchi dhidi ya idara ya mahakama."
Katika uamuzi wake wa Ijumaa, Jaji Mkuu David Maranga alisema kuwa uamuzi huo wa Mahakama ya Juu uliungwa mkono na majaji wanne kati ya sita na kuutangaza ushindi wa asilimia 54 wa Kenyatta kuwa batili.
Taarifa za kina juu ya uamuzi huo zitachapishwa hadharani ndani ya siku 21 tangu hukumu kutolewa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo