Ushindi huu wa tuzo ya amani kinachochea haja ya amani.
7 Oktoba 2016Rais wa Colombia Juan Manuel Santos amesema amepokea tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu kwa hisia kubwa. Wakati huo huo, hisia mbalimbali nazo zimejitokeza kuhusiana na kutunukiwa tuzo hiyo Juan Santos huku kiongozi wa wapiganaji wa FARC ambaye ni mshirika wa Santos kwenye mchakato wa amani akisema yeye tuzo anayotaka zaidi ni amani nchini Colombia.
Kutajwa kwake kuwa mshindi wa tuzo ya amani inayoheshimika ulimwenguni kote na yenye thamani ya dola laki tisa na elfu thelathini, ni mshangao kwa wengi hasa ikizingatiwa kwamba alishindwa kwenye kura ya maamuzi dhidi ya mkataba alioridhia wa amani unaolenga kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe Colombia.
Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo ya amani ya Nobel mwaka 2016 mapema leo, rais Juan Manuel Santos mwenye umri wa miaka 65, amesisitiza umuhimu wa tuzo hiyo kwa nchi yake na hasa kwa wale ambao wameathiriwa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka 50. Santos amesema "Hii ni heshima kuu kwa nchi yangu. Na kwa unyenyekevu, ninaipokea tuzo hii kwa niaba ya raia wa Colombia hasa waathiriwa. Ninasema shukrani tele. Tunahitajika tu kusukuma zaidi, kuvumilia nah ii itakuwa kichocheo kikuu ili tufike mwisho na tuanze ujenzi upya wa amani nchini Colombia "
Santos alitunukiwa tuzo hiyo kufuatia juhudi zake za kuendeleza mchakato wa kuhimiza amani nchini mwake, na kumaliza vita ambavyo vilisababisha vifo vya zaidi ya watu laki mbili na milioni sita kulazimika kupoteza makazi yao. Haya hapa maneno yake.
Hata hivyo wakosoaji wanasema kiongozi wa wapiganaji wa msituni FARC, na ambaye pia ni mshirika mkuu wa Santos katika mchakato huo wa kumaliza vita vya Colombia Rodrigo Londono pia alistahili kupewa tuzo hiyo, ili wawe washindi wawili. Rodrigo na rais Santos walitia saini mkataba wa makubaliano wa amani tarehe 26 Septemba, hivyo kutia kikomo mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe kwa miongo mitano iliyopita.
Kwenye ukurasa wake wa Twitter, kiongozi huyo wa FARC amesema, tuzo muhimu pekee anayotaka ni amani kwa raia wa Colombia, amani katika barabara za Colombia na amani isiyokuwa na ulipaji kisasi wala urongo. Mwenyekiti wa kamati inayochagua mshindi wa Nobel alipoulizwa mbona hawakumpa Rodrigo tuzo, Kaci Kullman alijibu "Kuna washirika wengi katika mchakato wa amani na rais Santos amekuwa akichukua hatua za kwanza muhimu na kihistoria. Kumekua na juhudi nyingi, lakini wakati huu anataka kushirikisha kila mmoja. Naye kama kiongozi wa serikali alikuwa mstari w ambele ndiyo sababu tukachagua rais wa Colombia"
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kutunukiwa rais Santos tuzo hiyo ni ujumbe maridhawa kwa watu wote wanaoshirikiana katika juhudi za upatanisho wa taifa. Ameongeza kuwa tuzo hiyo inawahimiza kuzidi kushirikiana hadi mchakato huo ukamilike, na kwamba kutofaulu kwa mkataba huo kwenye kura ya maamuzi iliyofanywa jumapili iliyopita, kusiwagawanye mamilioni ya raia
Tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2016 ilivutia jumla ya wawaniaji 376. Tuzo ya amani ya Nobel ilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1901. Hadi leo jumla ya tuzo 130 zimetolewa, 104 ikikabidhiwa watu binafsi na 26 kwa mashirika.
Tuzo hii hutolewa kwa mtu,au watu au hata taasisi zinazohusika katika kutoa mchango mkubwa kuleta amani katika jamii au duniani kwa Ujumla.
Mwandishi: John Juma/AFPE/DPE/RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu