Rais Jonathan awathibitishia Wakristo usalama wao
29 Desemba 2011Akizungumza baada ya kukutana na Jumuiya ya Makanisa ya Kristo nchini Nigeria, CAN, Rais Jonathan amesema kwamba iliyoshambuliwa ni Nigeria nzima na kwamba serikali yake haitachelea kuchukua hatua kwa yeyote anayehusika.
"Wacha niihakikishie tena Jumuiya ya CAN na Wanigeria wote kwamba, mashambulizi yoyote ya kigaidi dhidi ya raia au taasisi yoyote ya nchi hii, ni mashambulizi dhidi yetu sote, kwani magaidi hawana mipaka." Amesema Jonathan.
Kauli hii inaonekana kama jaribio la Rais Jonathan, kujaribu kutuliza jazba ya kidini inayoanza kupanda katika nchi hiyo iliyogawika baina ya Wakristo na Waislamu. Pia inachukuliwa kama jibu la serikali kwa Kanisa nchini Nigeria, baada ya Askofu wa Kanisa Katoliki, Ayo Oritsjafor kunukuliwa akisema sasa waumini wa Kristo nchini Nigeria wametangaziwa vita dhidi yao, na hivyo wana wajibu wa kujilinda kwa njia watakazoona zinafaa, pindi wakishambuliwa tena.
Miripuko kwenye maeneo ya makanisa nchini kote katika siku ya Krismasi iliwauwa watu wapatao 40 na kuwajeruhi wengine 60. Baadaye mashambulizi katika madrasa ya Kiislamu kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, yaliwajeruhi zaidi ya watu wanane, hali ambayo wachambuzi wanasema inaonesha ulipizaji kisasi.
Hata hivyo, Rais Jonathan amewaasa waumini wa dini zote mbili kuu nchini humo, kutokuiwachia nchi yao kuingia tena kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, kwani huko kutakuwa ni kukidhi matakwa ya magaidi. Badala yake amewataka Wanigeria kujitolea kupambana na kuwafichua magaidi hao.
"Magaidi ni watu kama sisi, si viumbe visivyoonekana. Wanaishi kama sisi na wanakufa kama sisi. Na ikiwa kweli Wanigeria tutajitolea, basi tutaweza kuwashinda." Amesema Rais Jonathan.
Mapema leo (29.12.2011), Jumuiya ya Kiislamu ya Ansaruddeen ya Nigeria, imesema kwamba mgogoro uliopo katika nchi hiyo si baina ya Waislamu na Wakristo, bali baina ya kundi moja la watu dhidi ya taifa zima. Kiongozi wa Jumuiya hiyo, Imam Abdul-Fattah Olustin, amesema kwamba Uislamu hauungi mkono mauaji ya maangamizi, mauaji ya kujitoa muhanga wala mauaji ya aina yoyote dhidi ya watu wasiokuwa na hatia.
Mara tu baada ya mashambulizi hayo hapo Jumapili, mufti mkuu wa Nigeria na ambaye ndiye pia Sultan wa Ukhalifa wa Sokoto, Saadu Abubakar, aliyalaani vikali akisema walioyafanya hawawakilishi mtazamo wa Waislamu.
"Tunataka kuwahakikishia ndugu zetu waumini wa dini ya Kikristo na Wanigeria wote, kwamba kilichojidhihirisha hapa si tafauti baina ya Uislamu na Ukristo, bali baina ya wema na uovu. Na watu wema ni wengi zaidi kwenye nchi yetu kuliko waovu, kwa hivyo tushirikiane sote kuwashinda waovu hao wachache." Alisema Sheikh Abubakar.
Wakati haya yakiripitowa, kuna taarifa kwamba Wakristo kwenye miji ya kaskazini ya Maiduguri, Damaturu, Potiskum na Kaduna wanaendelea kuihama miji hiyo kuhofia usalama wao. Televisheni ya Nigeria imesema kwamba kiasi ya watu 90,000 wameukimbia mji wa kaskazini mashariki wa Potiskum.
Ingawa hakujatangazwa amri ya kutotoka nje kwenye miji hiyo ya kaskazini, mashirika ya habari yanaarifu kuwa mikahawa, klabu za usiku na mabaa hufungwa na mapema kwani wateja wanaogopa kubakia maeneo hayo nyakati za usiku.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf