1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Hugo Chavez aaga dunia

Josephat Nyiro Charo6 Machi 2013

Rais wa Venezuela, Hugo Chavez, amefariki dunia leo (05.03.2013) baada ya kuugua saratani na hivyo kufikisha ukingoni uongozi wake wa miaka miwili katika taifa hilo la Amerika ya kusini lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

https://p.dw.com/p/17r37
NEW YORK - SEPTEMBER 20: Venezuelan President Hugo Chavez speaks during a news conference while attending the United Nations General Assembly September 20, 2006 at the UN in New York City.The annual conference comes at a contentious time for the world body as sanctions are being considered for Iran, while separately; UN peacekeepers are taking part in 18 operations around the world. (Photo by Spencer Platt/Getty Images)
Venezuela Hugo Chavez SWPicha: Getty Images

Makamu wa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ametangaza kupitia kituo cha televisheni nchini humo kuwa Chavez mwenye umri wa miaka 58 ameaga dunia na kusema kifo chake kimewaacha na uchungu mwingi.

Chavez amefariki katika hospitali ya kijeshi huko Caracass baada ya kuugua na kufanyiwa upasuaji mara nne uliosababisha afya yake kuzorota. Aligunduliwa kuwa na saratani ya tumbo mnamo mwezi Juni mwaka 2011 na amekuwa akifanyiwa matibabu nchini Cuba kabla ya kurejeshwa nyumbani.

CARACAS (VENEZUELA), 13/11/2011.- Venezuelan president Hugo Chavez, delivers his speech during the closing of a rally called by his electoral allies Gran Polo Patriotico (Great Patriotic Pole) in Caracas, Venezuela, 13 November 2011. Chavez said that there are terrorists infiltrated in Syria to generate violence, 'as they did in Libya', and exhorted his supporters to stay alert becuase 'everyday there are statements against Venezuela' from USA and its allies. EFE/Rodolfo Gutierrez
Marehemu Hugo ChavezPicha: picture-alliance/dpa

Mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, Chavez alishinda kirahisi muhula mwingine wa miaka sita kuliongoza taifa hilo kwenye uchaguzi mkuu lakini kutokana na hali yake mbaya ya afya hakuweza kuhudhuria shughuli ya kuapishwa kwake na hivyo kuilazimu mahakama ya juu nchini humo kuahirisha shughuli hiyo kwa mda usiojulikana.

Hisia za huzuni

Kifo chake kimewahuzinisha mamilioni wa wafuasi wake waliopendezwa na mtindo wake wa uongozi pamoja na sera zake kuhusiana na faida itokanayo na mafuta ya taifa hilo yaliyowapunguzia pakubwa mzigo wa gharama ya chakula na matibabu hasa kwa walioishi katika mitaa duni. Mamia ya wafuasi wa Chavez walikusanyika mbele ya hospitali alikofariki kiongozi huyo wakilia na kupiga kelele wakisema " Sisi sote ni Chavez"

Kumekuwa na hisia mbalimbali kote ulimwenguni kufuatia kifo cha Hugo Chavez, huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akitoa risala zake za rambirambi, "Amekuwa akitoa mchango wake katika maendeleo ya nchi yake. Wakati huo huo, kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ningependa kutoa risala za rambirambi kwa familia, raia na serikali ya Venezuela kwa kumpoteza rais Chavez."

UN chief Ban Ki-moon speaks during a press conference in Ankara, on December 7, 2012. UN chief Ban Ki-moon said on December 7 the use of chemical weapons by Syrian President Bashar al-Assad to combat the revolt would be an 'outrageous crime'. The UN chief, who flew to Turkey after visiting Jordan early Friday, repeated that he had written a letter to Assad urging him 'not to use under any circumstances chemical weapons' and warning him that 'it will create huge consequences.' AFP PHOTO/ADEM ALTAN (Photo credit should read ADEM ALTAN/AFP/Getty Images)
Ban Ki-moonPicha: AFP/Getty Images

Katika taarifa yake rais wa Marekani, Barack Obama, amesema, "Wakati huu mgumu Marekani inasisitiza kuwasaidia watu wa Venezuela na ari yake ya kuendeleza uhusiano wa maana na serikali ya Venezuela,Huku Venezuela ikianza ukurasa mpya katika historia yake. Marekani inaunga mkono sera zinazoimarisha kanuni za demokrasia, utawala wa sheria na kuheshimiwa kwa haki za binaadamu."

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amesema kifo cha Chavez ni janga kubwa na kwamba kiongozi huyo alikuwa mwanasiasa aliyesifika.

Kufuatia kifo cha rais Chavez, makamu wake ametangaza kuwa wanajeshi na polisi wamepelekwa kote nchini humo ili kulinda raia na kuhakikisha kuna amani, huku taifa hilo likiingia katika kipindi kigumu kisiasa na maombolezo.

Uchaguzi kufanyika

Kifo cha Chavez sasa kinatoa fursa ya kufanyika uchaguzi utakaodhihirisha kama mfumo wake wa uongozi wa kisosholisti utaandelea nchini humo bila yeye kuwepo. Uchaguzi unatarajiwa kufanywa katika siku 30 zijazo na kinyanganyiro kinatarajiwa kuwa kati ya makamu wa rais ambaye Chavez alimtaka kuwa mrithi wake wa kisiasa dhidi ya Henrique Capriles ambaye ni kiongozi wa upinzani aliyeshindwa na Chavez katika uchaguzi wa mwaka jana.

Miranda's Gov. Henrique Capriles waves to supporters after casting his ballot at a polling station in Caracas, Venezuela, Sunday, Dec. 16, 2012. Venezuelans are choosing governors and state lawmakers in elections that have become a key test of whether President Hugo Chavez's movement can endure if the socialist leader leaves the political stage. (AP Photo/Fernando Llano)
Henrique CaprilesPicha: dapd

Venezuela ina kiwango kikubwa zaidi cha mafuta duniani na hivyo wawekezaji watafuatilia kwa makini na kuwa na wasiwasi kuhusu kuyumba kwa taifa hilo kisiasa. Kushindwa kwa Maduro kutaleta mabadiliko makubwa nchini humo na kutaathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano wake na mataifa mengine ya Amerika kusini ambayo yalitegemea pakubwa ufadhili wa Chavez kutokana na mafuta hasa taifa la kikomunisti la Cuba ambalo liliweza kujikwamua kutoka hali mbaya kiuchumi katika miaka ya 90 kutokana na usaidizi wa Chavez.

Marekani yakanusha kuhusika

Wakati huo huo, Marekani imekanusha vikali madai ya kuwa ilihusika katika Rais Chavez kupata ugonjwa wa saratani na kuyataja madai hayo kuwa ya kuchekesha. Serikali ya Marekani ilitoa taarifa muda mfupi kabla kufariki kwa Chavez na kukanusha kuhusika kwa vyovyote vile na kifo cha Rais huyo kwa lengo la kulisambaratisha taifa hilo.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili haujakuwa mzuri kutokana na msimamo mkali wa kisosholisti wa Rais Chavez. Venezuela imetangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa na marehemu Chavez atazikwa Ijumaa ijayo.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/AFP/dpa

Mhariri: Josephat Charo