1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ghani ataka mazungumzo ya maana na Taliban

28 Januari 2019

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amewataka Wataliban kushiriki "mazungumzo ya maana" na serikali yake, baada ya waasi hao na Marekani kusifu maendeleo yaliofikiwa wakati wa majadiliano nchini Qatar wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/3CKbz
Afghanistan TV Ansprache Aschraf Ghani
Picha: Reuters/Afghan Presidential Palace office

Rais Ghani amesema pia kuwa uwepo wa wanajeshi wa kigeni nchini Afghanistan unatokana na makubaliano ya kimataifa na kwamba hawatahitajika katika kipindi cha muda mrefu.

Wataliban wamekataa kwa muda mrefu kuzungumza na serikali ya Afghanistan, wanayoitaja kuwa vibaraka. Lakini shinikio la miezi kadhaa la kidiplomasia kutoka kwa Marekani kuongoza mazungumzo lilipelekea mikutano ya siku sita kati ya Washington na waasi hao mjini Doha, na kuibua matumaini ya kupiga hatua, zaidi ya miaka 17 baada ya uvamizi wa Marekani.

Pande zote mbili - Wataliban na Marekani walisifu maendeleo yaliofikiwa mwishoni mw awiki, na gazeti la New York Times, limemnukuu mjumbe maalumu wa Marekani Zalmay Khalilzad Jumatatu, akisema wameunda rasimu ya mfumo, ingawa ameonya kuwa ufafanuzi zaidi unahitajika na kwamba masuala makuu yanayosababisha tofauti yanaendelea.

Afghanistan Zalmay Khalilzad in Kabul
Rais Ashraf Ghani akiwa katika mkutano na mjumbe maalum wa Marekani Zalmay Khalilzad mjini Kabul, Januari 28, 2019.Picha: picture-alliance/AA/Afghan Presidency Press Office

Masuala yanayozusha tofauti

Masuala hayo ni pamoja na usitishaji mapigano, ratiba ya kuondoka kwa vikosi vya kigeni, na hatua ya Wataliban kuendelea kukataa kuzungumza na serikali mjini Kabul.

Maafisa wa Afghanistan wamelalamika huko nyuma dhidi ya kutengwa katika mazungumzo hayo, na kuonya kuwa makubaliano yoyote kati ya Marekani na Wataliban yatahitaji ridhaa ya Kabul.

"Nawatolea mwito Wataliban kutoka nje ya mipango ya kishetani ya wageni, wakubali matakwa ya Wa Afghan na kuanza mazungumzo ya maana na serikali," alisema Ghani katika hotuba kwa njia ya Televisheni.

Ghani ametoa wito wa mazungumzo hapo kabla na alianisha mpango wa amani mwaka uliopita ambao ulihusisha usitishaji mapigano na kuwajumlisha waasi katika mchakato wa kisiasa.

Hawakujibu, ingawa mwezi Juni walikubali mpango wa usitishaji mapigano kwa siku tatu - wa kwanza katika kipindi chote cha mgogoro, hatua iliyopokelewa kwa shangwe huku wakionekana wakijichanganya na raia na kupiga nao picha maarufu kama "selfie" na kula nao ice creme.

Russland Vertreter der Taliban in Moskau
Kundi la Taliban likiwa limetengewa kiti katika mojawapo ya mikutano ya kimataifa.Picha: picture-alliance/Sputnik/V. Astapkovich

Nia ya mazungumzo

Khalilzad, ambaye amekuwa akiongoza majadiliano hayo, aliwasili mjini Kabul Jumapili jioni kuwaarifu maafisa wa serikali akiwemo Ghani kuhusu maendeleo yaliofikiwa.

Aliwahakikishia Waafghan kwamba mazungumzo nchini Qatar yanaendelea kunuwia kuwaleta waasi kwenye meza ya mazungumzo na serikali, kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya rais Ghani.

Ikulu ya Ghani imesema Khalilzad pia alithibitisha kuwa hakuna makubaliano yaliofikiwa kuhusu kuondolewa kwa vikosi vya kigeni, na kuongeza kuwa uamuzi wowote wa aina hiyo utaratibiwa na Kabul.

Wataliban wamesisitiza juu ya kuondolwa kwa vikosi vya kigeni. Marekani ndiyo inao wanajeshi wengi zaidi, wakifikia karibu elfu 14. Rais Donald Trump tayari amesema anataka kuondoa nusu yao.

Siku ya Jumamosi Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid alisema kwamba hadi ratiba ya kuondoka imeamuliwa, maendeleo kuhusu masuala mengine yatakuwa hayawezekani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/

Mhariri: Grace Patricia Kabogo