1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa umoja na kuvumiliana

14 Januari 2015

Viongozi wa kisiasa na kidini wa Ujerumani wametoa wito wa kuvumiliana katika ujumbe uliolenga kukabiliana na itikadi kali za dini na maandamano ya kuupinga Uislamu nchini kufuatia mashambulizi mjini Paris.

https://p.dw.com/p/1EJof
Mahnwache für Terroropfer am Brandenburger Tor 13.01.12014
Sote ni wamoja:Rais wa Ujerumani Joachim Gauck, mwenyekit wa Baraza la Waislamu Ayman Mazyek, Kansela Angela Merkel, naibu Kansela, Sigmar Gabriel wakionyeha mshikamano dhidi ya ugaidi.Picha: Reuters/F. Bensch

Kansela Angela Markel na rais Joachim Gauck walikuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ulioandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani, uliofanyika katika lango kuu la Brandeburg mjini Berlin, na kuwakumbuka pia wahanga 17 wa mashambulizi ya mjini Paris, yaliyofanywa na vijana wenye itikadi kali.

Uvumilivu na uwazi ndiyo yalikuwa maneno makuu ya mkutano huo wa jana Jumanne ulioendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo, "tuwepo kwa ajili ya kila moja wetu. Ugaidi: Siyo katika jina langu!" Akihutubia umati uliohudhuria mkutano huo, kiongozi wa baraza kuu la Jumuiya ya Waislamu wa Ujerumani Aiman Mazyek, aliwatolewa wito waumini wa dini zote kusimama pamoja dhidi ya vurugu na kutovumiliana.

"Tunatuma ujumbe wa wazi kutoka Berlin kwenda Ujerumani nzima na kwa ulimwengu. Kama ni dini au siyo, kama ni Myahudi, Mkristu au Muislamu, kinachotuunganisha ni kwamba tunapinga vurugu na kutovumiliana," alisema Mazyek na kuongeza kuwa "kwa pamoja tunawakilisha Ujerumani ya amani na ya watu wa rika zote, ambayo inatunza, kuheshimu na kulinda uhuru wa maoni na uhuru wa habari na uhuru wa dini. Sote ni Wajerumani."

Rais Joachim Gauck akihutubia mkutano wa mjini Berlin.
Rais Joachim Gauck akihutubia mkutano wa mjini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/Maurizio Gambarini/

Wahanga wa Paris wakumbukwa

Wanasiasa pamoja na viongozi wa vyama vya wafanyakazi, wafanyabiashara na wajumbe wa jamii za Wakristu na Wayahudi waliohudhuria mkutano huo, walinyamanza kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa mashambulizi ya wiki iliyopita mjini Paris.

Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck, alitumia hotuba yake katika mkutano huo kutuma ujumbe wa uhakikisho kwa Jamii ya Waislamu milioni nne wa Ujerumani, baada ya rekodi ya watu 25,000 kujiunga na maandamano yanayoongozwa na vuguvugu linaloupinga Uislamu. "Sote ni Wajerumani," alisema, na kusisitiza kuwa Ujerumani haitokubali kufarakanishwa na watu wa itikadi kali kutoka upande wowote.

"Ugaidi ni kitisho cha kimataifa, lakini cha kimataifa zaidi ni muungano wa walio huru na wanaotetea amani. Dunia inakuja karibu zaidi, kwa sababu uhuru na haki za binaadamu siyo vya Ufaransa, Ujerumani au Ulaya. Havikuja kwa bahati mbaya - ni vya ulimwengu wote," alisema rais huyo wa shirikisho la Ujerumani.

"Siyo katika jina langu," baadhi ya mabango ya washiriki wa mkutano huo yalisomeka.
"Siyo katika jina langu," baadhi ya mabango ya washiriki wa mkutano huo yalisomeka.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Hofu ya kukuwa kwa PEGIDA

Watu waliohudhuria mkutano huo walisifu ujumbe wake wa kuhimiza umoja wa dini mbalimbali ambao ulikuja baada ya maandamano ya 12 ya vuguvugu jipya la Ujerumani la mrengo mkali wa kulia- linalojiita Wazalendo wa Ulaya dhidi ya kusilimishwa kwa mataifa ya Magharibi- maarufu PEGIDA, ambalo limezaa makundi mengine madogo madogo nchini Ujerumani na hata nchini Norway.

Kansela Merkel, ambaye wiki hii alisisita kuwa Uislamu ni sehemu ya Ujerumani-- alisema mapema Jumanne kuwa chuki, ubaguzi na itikadi kali havina nafasi katika taifa hili. Naye rais wa Baraza kuu la Wayahudi nchini Ujerumani Abraham Lehrer, alisema haitakuwa sahihi kuwashuku Waislamu wote au kuikashifu dini yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi, lakini aliongeza kuwa ni juu ya Waislamu kukabiliana na hofu na ugaidi unaoenezwa na Waislamu wenye msimamo mkali barani Asia, Afrika na mashariki ya Kati.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape,dpae.

Mhariri: Daniel Gakuba