1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Donald Trump atoa hotuba ya kwanza kwa taifa

31 Januari 2018

Rais wa Marekani, Donald Trump amelihutubia taifa la Marekani katika hotuba yake ya kwanza ambapo amewataka Wamarekani wazingatie umoja wa kitaifa, mipaka yenye uthabiti na uwezo mkubwa wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/2rntf
USA Donald Trump Rede zur Lage der Nation
Picha: Reuters/W. McNamee

Rais Donald Trump miongoni mwa mambo mengine, amezungumzia juu ya kurekebisha miundombinu ya taifa na kurekebisha mfumo wa uhamiaji alioutaja kuwa umesambaratika.Rais huyo amelihutubia taifa kwa mara ya kwanza na kuielezea hali ya Marekani.

Wakati huo huo, rais Trump ametia saini amri mpya kwa ajili kuindeleza jela ya Guantanamo,hatua ambayo imebatilisha uamuzi rasmi wa mtangulizi wake Barack Obama aliyefanya jitihada za miaka minane kwa ajili ya kuifunga jela hiyo. Jambo hilo lilikuwa ni moja wapo katika ahadi alizozitoa Trump wakati wa kampeni yake alisema anataka jela ya Guantanamo ibakie wazi na itumiwe kwa kuwazuia watu wabaya, ijapokuwa yeye mwenyewe bado hajampeleka mtu yeyote kwenye jela hiyo.

Jela ya Guantanamo
Jela ya GuantanamoPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Fox

Trump aliitia saini amri hiyo kabla ya kutoa hotuba yake ya kwanza kwa taifa la Marekani ambapo amesema Marekani bado ina uwezo wa kuwazuia maadui kwa kuwaweka kwenye jela hiyo ya Guantanamo iliyopo nchini Cuba kwa ajili ya kulinda usalama wa taifa la Marekani. Amesema waziri wa ulinzi atahitajika kutoa mapendekezo ya vigezo vitakavyotumika kuamua hatima ya watu waliotekwa na Marekani katika vita, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka Guantanamo.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/L. Millis

Trump aliitumia hotuba yake kujaribu kuonyesha ustadi katika uongozi wake kama rais kwa ajili ya kuwaondoa watu wanaotilia mashaka urais wake wakati anapokabiliwa na uchunguzi kuhusu mahusiano yake na Urusi wakati wa kampeni huku akiteseka kwa kushindwa kupata alama nzuri kuhusiana na suala la kupatikana ajira kwa sababu hali hiyo bado haijabadilika licha ya kwamba yeye mwenye anajisifu. Amesema tangu kumalizika kwa uchaguzi serikali yake imefanikiwa kutenga nafasi mpya za kazi milioni 2.4 ikiwa ni pamoja na ajira mpya 200,000 katika viwanda peke yake.

Hata hivyo hotuba ya Rais Trump isingekamilika bila kuitaja Korea Kaskazini. Trump amewaambia Wamarekani kuwa mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini unaweza kuhatarisha nchi ya Marekani ambapo ameapa kuendeleza kampeni dhidi mpango wa silaha za nyukliaili wa nchi hiyo.

Mwanasiasa Bernie Sanders
Mwanasiasa Bernie SandersPicha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Mwanasiasa wa Marekani Bernie Sanders ameikosoa hotuba ya Trump kwa kile ambacho amesema trump hakuyasema mengi katika hotuba yake kama masuala ya usalama na bima ya afya licha ya ahadi wakati wa uchaguzi kwamba angeurekebisha na kuulinda mpango huo maarufu.

Seneta huyo wa jimbo la Vermont pia ametaja tofauti zilizopo kati ya matajiri na masikini pamoja na masuala ya hali ya hewa. Amesema Trump ameshindwa kukabiliana na vitisho vya msingi na hata kuvishughulikia. Mwanasiasa huyo Sanders bado anatafakari iwapo atagombea urais mwaka 2020.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE/AFPE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo