Rais Donald Trump ahutubia bunge kwa mara ya kwanza
1 Machi 2017Ni hotuba iliyokuwa imengojewa kwa hamu hadi pale rais wa Marekani aliposimama mbele ya bunge na kulihutubia. Hata hivyo hotuba ya Trump ilielemea zaidi katika maswala ya uhamiaji na kuwapunguzia kodi wananchi. Lakini hotuba ya rais huyo wa Marekani haikugusia maswala ya soko la fedha kama ilivyotarajiwa na wawekezaji na wafanya biashara.
Rais huyo wa Marekani Donald Trump katika hotuba yake hata hivyo alionyesha kidogo kulegeza msimamo wake juu ya wahamiaji haramu. Katika hotuba yake aliwaambia wajumbe kwamba yuko tayari kwa mageuzi katika swala zima la uhamiaji. Hotuba yake ilionekana kuhama kwenye matamshi makali juu ya maswala ya uhamiaji ambayo alikuwa akiyatoa wakati wa kampeni. Ilikuwa tofauti mwezi mmoja baadae tangu alipoapishwa na kuingia ikulu.
Aliwaambia wabunge kwamba anaamini inawezekana kufanya mabadiliko katika sera ya uhamiaji na kwamba kuwalinda wafanyakazi wa Marekani kunamaanisha kufanyiwa marekebisho katika mfumo huo. Rais Trump alitolea mfano nchi kama Canada na Australia ambazo alisema zina mifumo bora ya uhamiaji. Lakini baadhi ya wajumbe wa chama cha Republican wanapinga hatua anazotaka kuzichukua rais huyo wa Marekani kama kupunguza kwa kiwango kikubwa misaada ya Marekani kwa nchi za kigeni. Kiongozi wa Seneti Mitch McConnell ambaye aliwahi kuongoza jopo lililosimamia bajeti ya misaada ya nje amesema haungi mkono kupunguza bajeti ya misaada ya nje. Rais Donald Trump katika mpango wake analenga kupunguza misaada ya nje na badala yake kuiongezea wizara ya ulinzi kiasi cha dola bilioni 54. Hatua hiyo itakuwa inapunguza kwa asilimia 37 fedha kutoka kwenye wizara za mambo ya ndani na ile ya diplomasia na mambo ya nje. Punguzo hilo bila shaka litaleta ugumu usiofichika katika wizara hizo husika.
Mkurugenzi wa maswala ya bajeti wa rais Donald Trump Mick Mulvaney amesema anachotaka kukifanya rais Trump ni kupunguza matumizi ya nje na badala yake kuzirejesha fedha hizo kwa ajili ya matumizi ya ndani. Katika hotuba yake hiyo ya kwanza rais Donald Trump alizungumzia juu ya vyombo vya habari, maswala ya biashara ambapo alisema haungi mkono sera ya kulinda dhidi ya bidhaa zinazoingizwa Marekani. Alikumbusha juu ya kuzilinda ahadi alizozitoa kwa Wamarekani.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE/RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu