1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Chavez atangaza kuiondoa Venezuela kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa

1 Mei 2007

Rais Hugo Chavez wa Venezuela ametangaza kuwa nchi yake itajitoa kutoka kwenye Benki ya Dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF. Rais Chevez amesema kuwa nchi yake haihitaji kuwa na mwakilishi kwenye mashirika hayo.

https://p.dw.com/p/CB4N
Rais Hugo Chavez wa Venezuela
Rais Hugo Chavez wa VenezuelaPicha: AP

Rais huyo ambaye kwa muda wote amekuwa katika mkondo wa dafurao na Marekani , yenye usemi mkubwa katika taasisi hizo amesema anataka kukamilisha matayarisho ya kujiondoa kwenye mashirika hayo.Amezilaumu taasisi hizo kwa alichoita kuzinyonya nchi zinazoendelea.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kiongozi huyo wa Venezuela aliwaambia wananchi wake, kuwa Venezuela haina haja ya kuwa na mwakilishi kwenye mashirika hayo yanayowakilisha maslahi ya kibeberu ya Marekani.

Rais Chavez amemwagiza waziri wake wa fedha aanze kushuhgulikia hatua za kuiwezesha Venezuela kuondoka Benki ya Dunia na shirika la fedha la kimataifa.

Tangazo la rais wa Venezuela halikuja kama jambo la kushangaza .Raisi huyo anatetea sera za mlengo wa kisoshalisti.Hivi karibuni alizungumzia juu ya kuilekeza nchi yake kwenye njia ya kuwa jamhuri ya kisoshalisti.

Siku mbili kabya ya kuapishwa kuwa rais kwa kipindi cha tatu bwana Chavez alitaifisha kampuni za nishati na mawasiliano ya simu.Rais huyo alisema wakati huo kuwa Venezuela inapasa kudhibiti utajiri wake.

Rais Chavez amesema nchi yake itadai irudishiwe fedha ilizokuwa inatoa kama mchango kwenye shirika la IMF na Benki ya Dunia.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanatathmini uamuzi wa rais Chavez kuwa sehemu ya shabaha anayolenga katika kuanzisha benki ya kusini itakayofadhili miradi ya maendeleo katika nchi za Amerika ya kusini.

ABDU MTULLYA