1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush akaribishwa Vatican

Kalyango Siraj13 Juni 2008

Atakutana na Sarkorzy mjini Paris

https://p.dw.com/p/EJIc
Papa Benedict XVI na rais George W. Bush wakati wa ziara ya Baba Mtakatifu nchini Marekani miezi kadhaa iliopita.Rais Bush nae leo Ijumaa 13.06.08 amekwenda VaticanPicha: picture-alliance / dpa

Rais George W. Bush wa Marekani anayeendelea na ziara yake barani Ulaya inayotajwa kuwa ya mwisho kabla hajamaliza mda wake mwishoni mwa mwaka huu,leo Ijumaa alikaribishwa katika makao makuu ya Vatican na kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani papa Benedict wa kumi na sita.

Rais Bush alikuwa na mazunguzo ya dakika 30 na Papa Benedikti.

Ulinzi ulikuwa mkali na polisi pamoja na makamando wa kupambana na ugaidi walitanda katika sehemu za karibu na eneo hilo.

Bush alimuelezea Papa Benedict,wa kumi na sita, kwamba kukutana nae ilikuwa ni heshima.

Baada ya mazungumzo yao walisimama kwenye ukuta wa majengo ya kale katika uwanja wa mtakatifu Petro.

Taarifa iliotolewa na Vatican baadae imesema kuwa viongozi hao wawili wamejadilia kile kilichoitwa ulinzi wa maadili,mashariki ya Kati na suala la amani katika eneo takatifu la mshariki ya kati.Pia masuala ya utandawazi na mgogoro wa chakula hayakupigwa kisogo,imesema taarifa.

Ziara ya rais bush nchini Italy ilikuwa ya siku tatu na mbali na kukutana na Papa Benedikt pia amekutana na rais Giorgio Napolitano na waziri mkuu Silivio Berlusconi.

Baada ya kukutana na waziri mkuu Berlusconi,rais Bush alisema kuwa wote kwa pamoja wanahitajika kuta ujumbe mmoja kwa Iran ukiitaka kukomesha hatua zake za mpango wa urutubishaji la sivyo itakabiliwa na vikwazo zaidi.

Mda hiyo anatarajiwa kuendelea nayo katika ziara yake hii katika nchi za Uingereza na Ufaransa ambako ndiko kituo chake kingine.

Rais Bush akiwa Ufaransa atazamiwa kutoa hotuba ya buriani katika mkutano wa shirika la kuichumi na maendeleo-OECD ambao unafanyika mjini Paris.

Pia anatarajiwa kurejelea mwito wake wa kuizuia Iran kutengeneza bomu la nuklia na vilevile kutafuta uungwaji mkono wa juhudi zake za kutaka demokrasia kutia mizizi katika eneo la mashariki ya kati.

Ili kuweza kutafuta kuungwa mkono katika sera yake kuhusu Iran,rais Bush atakutana na rafiki wake wa karibu rais wa Ufaransa,Nicholas Sarkorzy leo na kesho kabla ya kukutana pia na waziri mkuu wa Uingereza,Gordon Brown,mjini London jumamosi na jumapili.

Bw Bush ameendela na mada yake hiyo ya kuitilia guu Iran katika ziara yake ya Ulaya ambayo imempeleka Slovenia,Ujerumani,Italy na sasa Ufaransa na baadae Uingereza.