Rais Buhari: Mwaka mmoja madarakani
29 Mei 2016Wapiga kura waliokuwa na matumaini makubwa walimpa Buhari nguvu ambayo haikuwa na mtihili ya kupambana na Rais aliekuwamo madarakani Goodluck Jonathan wakati wa uchaguzi.
Katika historia ya Nigeria, hapakuwapo mgombea wa upinzani alieshinda.Buhari ni wa kwanza.
Serikali ya Rais Jonathan ikikuwa na mapungufu katika kuyatekeleza majukumu yake kiasi kwamba wananchi wa Nigeria walitumai kuyaona mageuzi waliyoahidiwa na Buhari. Na laiti ingeliwezekana walitaka kuyaona mabadiliko hayo mara moja , katika sekta zote na kwa mpigo.
Rais Buhari hakuweza kuyatimiza malengo makubwa aliyoyaweka kwa sababu , aliahadi masuluhisho ya haraka katika masuala muhimu, ikiwa pamoja na kuwashinda magaidi,kukomesha rushwa na kuondoa bughudha ya katikakatika ya nishati ya umeme.
Aliahidi kuyatatua matatizo hayo mara moja na yaingie katika kapu la sahau.
Mafanikio katika kupambana na ugaidi
Kuhusu ugaidi Buhari ameweza kuwarudisha nyuma magaidi wa Boko Haram, lakini magaidi hao bado wapo na hakika Buhari mwenyewe amekiri kwa njia ya kufanya mabadiliko katika uongozi wa jeshi na ameweza kukomesha ufisadi katika taasisi hiyo.
Jeshi la Nigeria lilifanikiwa,katika muda wa miezi michache kuwatimua magaidi wa Boko Haram katika karibu sehemu zote walizokuwa wanazidhibiti.Katika juhudi hizo jeshi la Nigeria liliweza kuwakomboa mamia ya raia waliotekwa nyara na Boko Haram.Lakini kutokana na kubanwa na kuanza kutapatapa magaidi wa Boko Haram walihamia katika mkakati wa mashambulio ya kujitoa mhanga kwenye miji na vijiji.
Wasichana waliotekwa nyara katika mji wa Chibok bado hawajapatikana. Mpaka leo ni mmoja tu alierejea nyumbani.Katika harakati za kupambana na magaidi wa Boko Haram, Rais Buhari anaweza kuhesabu mafanikio mengi. Lakini bado hajashinda kabisa vita hivyo.
Buhari pia aliahidi kulinda haki za binadamu. Alisema chini ya uongozi wake majeshi ya usalama yanayochukiwa na wananchi yatazitekeleza haki za binadamu. Hata hivyo mpaka sasa bado hatua kubwa haijapigwa katika suala hilo.
Na kwa kweli zipo habari juu ya kukamatwa kiholela kwa watu wanaotuhumiwa kuwa magaidi. Na mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema wale ambao siyo watiifu ,na wale wanaoikosoa serikali wanazingatiwa kuwa wasaliti. Mnamo mwaka 2015 Waislamu 300 wa madhehebu ya kishia waliangamizwa.
Rais Buhari anapaswa kuyapa masuala hayo kipaumbe. Bado anayo kazi kubwa ya kuifanya.
Pia katika sekta ya uchumi Buhari lazima avae njuga. Bidhaa kuu za kuingizia mapato ni mafuta na gesi. Fedha za kigeni zimepungua nchini Nigeria sasa kutokana na bei ya mafuta kuanguka kwenye soko la dunia. Sarafu ya Nigeria imeanguka thamani.
Utawala wa Buhari unakataa kuiachia Naira iwe na thamani katika msingi wa miamala ya soko. Hali hiyo inasababisha mgogoro mkubwa zaidi katika upatikanaji wa fedha za kigeni.
Wananchi bado wana inami na Buhari
Lakini anapotimiza mwaka mmoja madarakani, Rais Buhari anaweza kujivunia mafanikio aliyoyapata katika kupambana na rushwa. Maafisa wakubwa na wadogo wamenaswa.
Sura ya Nigeria pia imekuwa nzuri kutokana na ziara za Rais Buhari katika nchi za nje. Ndiyo sababu Marekani inakusudia kuiruhusu Nigeria kununua tena silaha kutoka nchi hiyo. Na mafanikio makubwa zaidi ni kwamba watu wa Nigeria bado wana imani na Rais Muhammadu Buhari .
Mwandishi:Mösch Thomas.
Mfasiri.Mtullya Abdu.