1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Buhari amjibu Cameron kuhusu rushwa

Admin.WagnerD11 Mei 2016

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amesema nchi yake haina haja ya kumtaka Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron aombe radhi kwa kuiita Nigeria kuwa nchi yenye ufisadi mkubwa sana

https://p.dw.com/p/1IltE
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/dpa/W. Krumm

Waziri Mkuu wa Uingereza alirekodiwa akisema kuwa huenda Nigeria na Afghanistan zikawa nchi zilizokithiri katika rushwa duniani. Cameron aliyasema hayo kwenye halfa iliyofanyika kwenye kasri ya Buckingham mjini London alipokuwa anaongea na Askofu Mkuu wa Canterburry Justin Welby.

Kauli ya Cameron imefichuliwa kabla ya mkutano wa viongozi wa dunia utakaofanyika kesho mjini London kuzijadili njia za kupambana na ufisadi.Cameron, atakayekuwa mwenyeji wa mkutano huo hakujuwa kwamba alikuwa anarekodiwa.

Akijibu kauli ya Cameron Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameitaka Uingereza izirejesha mali za Nigeria zilizoibwa na kufichwa Uingereza.

Rais Buhari alikumbusha juu ya mkasa wa aliekuwa Ganava wa jimbo tajiri la mafuta Diepreye Alamieyeseigha aliekatamwa mjini London. Alamieyeseigha aliefariki mwaka uliopita, nchini Nigeria aliacha akaunti ya benki ya kudumu pamoja mali nyingine

Uingereza iko tayari kurudisha mali za Nigeria

Rais Buhari amesema Uingereza iko tayari kuzirudisha mali za mtu huyo nchini Nigeria. Ameeleza kuwa hicho ndicho ambacho Nigeria inakitaka badala ya kuitaka Uingereza iombe radhi.

Marehemu gavana huyo alitoroka kwa kujifanya aonekane kama mwanamke, baada ya kupewa dhamana.Alifunguliwa mashtaka kwa kuekeza fedha haramu.

Tangu aingie madarakani Rais Buhari ameanzisha kampeni ya kupambana na rushwa nchini Nigeria na katika hotuba yake leo pia ameishukuru Uingereza kwa kusaidia katika juhudi za kuzirudisha mali za Nigeria zilizoibwa na kufichwa nchini Uingereza. Buhari amesema hata kabla ya yeye kuingia madarakani Uingereza ilikuwa inawakamata magavana wa zamani waliokimbilia katika nchi hiyo.

Afghanistan ambayo pia imeitwa na Waziri Mkuu Cameron kuwa nchi yenye ufisadi mkubwa sana nayo imemjibu Waziri Mkuu huyo.

Mbunge wa nchi Mohammad Farhad Sediqi amesema ufisadi upo nchini Afghanistan.Lakini Ungereza, Marekani na Jumuiya ya kimataifa zimeshiriki katika kuujenga na kuueneza nchini Afghanistan.

Mbunge huyo ameeleza kuwa kabla ya kuanza mkutano juu ya kupambana na rushwa kauli ya Waziri Mkuu wa Uingereza ni kebehi kwa Afghanistan.

Mkutano wa kesho unaohudhuriwa na viongozi kutoka nchi zaidi ya 60 ikiwa pamoja na Tanzania una lengo la kuhamasisha juhudi za kupambana na rushwa katika nyanja zote za maisha.

Mwandishi:Mtullya abdu. afp,dpae

Mhariri:Gakuba Daniel