Rais Barack Obama atunukiwa zawadi ya amani ya Nobel
10 Desemba 2009Barak Obama amepokea hii leo tuzo ya amani ya Nobel kwa "unyenyekevu" akisema kuna wengine waliostahiki zaidi kuliko yeye.
Tuzo hiyo ya amani ya Nobel ametunukiwa rais Barack Obama ,siku chache tuu baada ya kuamua kuimarisha juhudi za vita nchini Afghanistan.
"Nnaamini kuna wengine ambao pengine wamestahiki zaidi kuliko mie" amesema rais Obama wakati wa mazungumzo na waandishi habari pamoja na waziri mkuu wa Norway Jens Stoltenberg,kabla ya kupokea zawadi ya amani "kwa shukurani za dhati na unyenyekevu" wakati wa sherehe rasmi zilizofanyika katika kasri la meya wa Oslo.
Hata kabla ya kupitisha mwaka mmoja madarakani,huku akikabiliana na vita viwili vinavyopamba moto nchini Irak na Afghanistan,na bila ya kufanikiwa sana katika uwanja wa kidiplomasia,rais huyo wa 44 wa Marekani aliwashangaza wengi alipoteuliwa kama mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel ya mwaka huu.
Kabla ya kumkabidhi tuzo hiyo ambayo ni medali na shahada yenye thamani ya yuro karibu milioni moja,mwenyekiti wa kamati ya Nobel Thorbjoern Jagland alijaribu kusawazisha lawama za wale wanaodai ni mapema kwa Obama kutunukiwa zawadi hiyo.
„Kuna wengi wanaohisi ametunukiwa mapema zawadi hii.“ Amesema Thorbjoern Jagland aliyekumbusha :“Historia imejaa fursa zilizopita bure.Ni sasa,leo ambapo tumepata fursa ya kuunga mkono fikra za rais Obama-amesema na kufafanua tuzo hiyo ni mwito wa kuendelezwa juhudi kwa pamoja.“
Katika mkutano na waandishi habari,rais Barack Obama ameahidi kuendelea na siasa yake:kuimarisha amani na usalama ulimwenguni,kuleta utulivu nchini Afghanistan,kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuzidisha juhudi za kuitakasa dunia na silaha za kinuklea.
Rais Barak Obama amesema:
„Ni kweli pia kwamba usalama hauwezi kupatikana ikiwa binaadam hawana njia za kupata chakula au maji safi ya kunywa,au madawa na mahala pa kuishi.“
Katika hotuba yake rais Barack Obama amesema vita wakati mwengine vinajitokeza kua muhimu,huku akisisitiza gharama zinazotokana na vita hivyo.
Makundi kadhaa ya wanaharakati wanaopinga vita wametundika biramu karibu na jengo la taasisi ya Nobel yenye maandishi yasemayo:"Obama umetunukiwa zawadi ya amani ya Nobel,jitahidi uistahiki."
Katika kuta za taasisi hiyo,picha ya rais wa Marekani imekuja kuchanganyika na zile za washindi wengineo mfano Nelson Mandela,Mama Theresa na Martin Luther King
Norway ambayo kawaida ni nchi tulivu imeimarisha hatua za usalama jambo ambalo halijawahiu kushuhudiwa nchini humo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Reuters/AFP)
Mhariri:Abdul-Rahman