1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila aapishwa kuwa "rais wa wananchi" Kenya

30 Januari 2018

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga aliapishwa Jumanne kuwa rais wa wananchi wa Kenya, katika hatua ya kupinga muhula mpya wa rais Uhuru Kenyatta baada ya miezi ya machafuko ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/2rmte
Kenia "Vereidigung" von Raila Odinga in Uhuru Park in Nairobi
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga akionyesha ishara kwa wafuasi wake wakati akiwasili kwa ajili ya kuapishwa kama "rais wa wananchi" Jumanne, 30.01.2018.Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Serikali  ilizima  matangazo  ya  moja  kwa  moja  ya  vituo vitatu  vikuu  vya  televisheni  wakati  kundi  kubwa  la  watu kwa  maelfu  wakikusanyika  katika  uwanja  wa  Uhuru Park  mjini  Nairobi  kuhudhuria kuapishwa kwa Odinga.

Licha ya kwamba polisi waliondolewa bila ya maelezo katika  uwanja  wa  Uhuru  Park, polisi  wengi  walibakia katika maeneo ya mabanda katika mji huo, ambayo ni ngome kuu ya upinzani.

Odinga  alisema  amejikuta katika hali ya kutokuwa na usalama wakati akihudhuria tukio hilo la  kula kiapo baada ya walinzi wake kuondolewa. 

Odinga  mwenye  umri  wa  miaka  73 alikula  kiapo  akiwa ameshika  biblia  huku  watu  wakishangiria. Kiongozi  huyo wa  upinzani  ameiita  sherehe  hiyo  kuwa  ni  hatua  moja mbele  kuelekea  kupatikana  kwa  demokrasi inayofanyakazi  nchini  Kenya.

"Tunashuhudia kurejea kwa utawala wa kiimla, urais wa kibepari nchini mwetu na utawala wa amari, na hayo laazima yapingwe," alikiambia kituo cha utangazaji cha KTN kabla ya kuelekea kwenye hafla ya kuapishwa.

Kenia Nairobi Großdemonstration der Opposition
Wafuasi wa muungano wa upinzani NASA, wakikusanyika kushuhudia kiongozi wao Raila Odinga akila kiapo cha kuwa rais wa wananchi, Jumanne, 30.01.2018.Picha: Reuters/B. Ratner

Baadae alirekebisha maelezo yake kwenye ukurasa wa twitter na kujiita "Rais wa Jamhuri ya Kenya."

National Resistance Movement marufuku

Saa kadhaa baadae serikali ikalipiga marufuku vuguvugu la taifa la upinzani, ambapo waziri w amambo ya ndani Fred Matiangi alilitangaza kuwa kundi la uhalifu.

Kwa mujibu wa sheria ya Kenya, kuwa mwanachama wa kundi la uhalifu wa kupanga inaweza kukupelekea kufungwa gerezani kwa muda usiyozidi miaka kumi, faini ya dola za Marekani zisizozidi 5,000 au vyote viwili.

Hafla hiyo ya dhihaki ilikuja baada ya miezi kadhaa ya mashaka ya kisiasa. Mahakama ya juu kabisaa nchini Kenya ilibatilisha uchaguzi wa mwezi Agosti, baada ya Odinga kudai kwamba wadukuzi wa mtandaoni waliingilia mitambo ya computer ya tume ya uchaguzi na kubadilisha matokeo kumpendelea Kenyatta.

Hukmu hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa mahakama kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais barani Afrika. Mahakama iliezea kasoro na ukiukaji wa sheria na kuamua dhidi ya Kenyatta kwa sababu tume ya uchaguzi ilikataa kufungua mfumo wake wa computer kutathminiwa.

Kenia "Vereidigung" von Raila Odinga in Uhuru Park in Nairobi
Wafuasi wa Raila Odinga wakimsikiliza kiongozi wao akila kiapo cha kuwatumikia katika Bustani ya Uhuru mjini Nairobi, Jumanne 30.01.2018.Picha: Reuters/B. Ratner

Matokeo halisi ya uchaguzi

Wiki iliyopita upinzani ulitoa kile ulichokitaja kuwa matokeo sahihi yakionyesha kuwa Odinga alishinda uchaguzi wa Agosti, lakini ulikataa kusema ni kwa namna gani ulipata taarifa hizo kutoka mifumo ya computer za tume ya uchaguzi. Tume ya uchaguzi iliyataja matokeo hayo kuwa ya "bandia."

Awali polisi iliapa kuwazuwia wafuasi wa upinzani kuhudhuria sherehe ya Jumanne, na kuzusha hofu ya kutokea vurugu. Tume ya haki za binadamu inayofadhiliwa na serikali ya Kenya imesema watu wasiopungua 92 waliuawa na dazeni kadhaa wengine walishambuliwa kingono wakati wa miezi ya vurugu za uchaguzi. Wengi wao walikuwa wafuasi wa upinzani.

Watetezi w ahaki za binadamu wanautuhumu utawala wa Kenyatta kwa ukiukaji wa uhuru unaodhaminiwa na katiba, ukiwemo wa kukusanyika na kujieleza.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Mohammed Abdulrahman