1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Zimbabwe wapiga kura leo.

Josephat Charo30 Machi 2005

Zimbabwe inawategemea waangalizi wa Afrika kuyaidhinisha matokeo ya uchaguzi wa leo, ili kuepuka lawama kutoka mataifa ya kigeni na kuyafanya matokeo hayo yaheshimike.

https://p.dw.com/p/CEG6
Mmoja wa wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC, nchini Zimbabwe.
Mmoja wa wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC, nchini Zimbabwe.Picha: AP

Rais Robert Mugabe ana hamu kubwa kuudhihirishia ulimwengu kwamba ameboresha sera yake ya maongozi ya kidemokrasi tangu uchaguzi wa mwaka wa 2000 na 2002, uliogubigwa na machafuko na shutuma za udanganyifu. Alisema uchaguzi huu wa bunge utakuwa huru na wa haki na hapo jana alitangaza kwamba ataunda serikali ya umoja wa taifa itakayowajumulisha viongozi wa upinzani, iwapo chama chake cha ZANU-PF kitashinda katika uchaguzi wa leo.

Lakini umoja wa Ulaya tayari imeutaja uchaguzi huo kuwa bandia huku Marekani ikisema matokeo yake hayawezi kuaminiwa kwani tayari yametayarishwa kuipendelea serikali. Zimbabwe imewaalika waangalizi wa uchaguzi, wengi wao kutoka mataifa ya Afrika, umoja wa Afrika na kamati ya maendeleo ya mataifa ya kusini mwa Afrika, SADC, ambayo ilimuunga mkono Mugabe alipokabiliwa na madai ya wizi wa kura wakati wa uchaguzi mkuu wa 2002.

Serikali ya Harare ilikataa kuwaalika waangalizi kutoka Marekani, Uingereza au Australia na makundi mengine kama vile jumuiya ya madola na umoja wa Ulaya. Mugabe anasema mataifa ya magharibi yaliuhukumu uchaguzi huo hata kabla kufanyika kwa sababu ni katili kwa serikali yake.

Zimbabwe iliwapa idhini waandishi habari zaidi ya 200 wa kigeni, lakini ikawakataza wengine wengi, wakiwemo watangazaji kutoka Marekani, Uingereza na Australia. Pia iliyafungia nje makundu muhimu kama vile baraza la bunge la SADC, ambalo lilikataa kuyaidhinisha matokeo ya uchaguzi wa 2002.

Ayesha Kajee, mtafiti katika taasisi ya maswala ya kimataifa mjini Johannesburg, Afrika Kusini, amesema Zimbabwe inataka iaminiwe, lakini makundi yaliyoruhusiwa kuingia nchini humo hayawezi kutoa ripoti itakayoweza kuaminiwa kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

Naye Nel Marais, mchambuzi kutoka mjini Pretoria aliongeza kusema rais Mugabe anajua hawezi kuwa na uchaguzi pasipo kuwahusisha waangalizi wa mataifa ya kigeni na tayari amefanikiwa kuyahimiza makundi kadhaa kumuunga mkono kwamba aliyazingatia makubaliano ya SADC.

Marais alisema hakuna waangalizi walioruhusiwa kuingia Zimbabwe siku 90 kabla ya uchaguzi wa leo, kama ilivyotakikana na SADC. Hatua hii ilipunguza uwezo wao wa kutathmini ikiwa viongozi wa upinzani walipewa wakati wa kutosha katika radio na televisheni ya kitaifa.

Kwa upande mwingine wafuasi wengi wa kiongozi wa upinzani, Morgan Tsvangirai wameanza kutafakari uwezo wa kiongozi huyo kuweza kuiongoza Zimbabwe. Morgan Tsvangirai, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC, alionekana kuwa tumaini kubwa kwa upinzani wa Zimbabwe, shujaa aliyekuwa na nafasi nzuri ya kumshinda rais Robert Mugabe. Lakini sasa wafuasi wa chama chake wanatafakari kuhusu uwezo wa kiongozi huyo kuweza kuliongoza taifa hilo.

Chama cha MDC, ambacho wafuasi wake wamevunjwa moyo na mbiyo wa serikali ya rais Mugabe, kina nafasi ndogo ya kushinda katia uchaguzi wa leo. Wadadisi wa kisiasa wanasema ijapokuwa Tsvangirai amekosa nafasi muhimu za kuwa rais wa taifa hilo, na pengine alidanganywa katika uchaguzi wa rais miaka mitatu iliyopita, bado anaonekana kama shujaa na wazimbabwe wengi kwa kupambana na rais Mugabe.

Tsvangirai, katika kampeni yake ya uchaguzi alizangatia maswala ya kuwapa chakula raia wa Zimbabwe wanaoteseka kwa njaa, kupunguza ukosefu wa ajira na kuufufua uchumi ambao wakati wa uhuru kulikuwa na matumaini makubwa ya kunawiri.

Wafuasi wake na mataifa mengi ya kigeni yalimtazama kama tumaini la pekee la Zimbabwe kuweza kujikwamua kutokana na uchumi uliozorota na mzozo wa kisiasa. Lakini wadadisi wanasema chama cha MDC kimekumbwa na mizozo kati ya wanachama wake na maongozi yake yamesambaratika, kiasi kwamba hakiwezi kuchukua hatamu za uongozi wa taifa kutoka kwa chama cha ZANU-PF.

Ama kweli leo ni leo msema kesho ni muongo, kwani kura ya leo ndiyo itakayoamua ni nani atakayeiongoza Zimbabwe.