1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Zimbabwe wakimbilia nchini Afrika Kusini.

6 Mei 2008

Hali ya kisiasa na kiuchumi nchini Zimbabwe imewafanya raia wengi wa nchi hiyo kukimbilia nchi jirani ya Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/DucL
Rais Robert Mugabe,wa Zimbabwe akipiga kura yake siku ya Uchaguzi uliofanyika mjini Harare, March 29, 2008.Picha: AP

Watu hao wengi wao wamekuwa wakipata hifadhi katika kituo kimoja cha kidini cha Madhehebu ya Kimethodist kilichoko Mjini Johannesburgh.

Usiku kucha kila siku, maelfu ya wakimbizi kutoka nchini Zimbabwe ambao wameikimbia nchi yao kutokana na kushuka kwa uchumi wa nchi hiyo pamoja na mambo ya Kisiasa wamekuwa wakiingia nchini Afrika Kusini.

Mwalimu mmoja wa Sekondari anayefundisha masomo ya hesabu na sayansi kutoka mji wa Chitungwiza ulioko Kusini mwa mji Mkuu wa Zimbabwe, Harare, Owen Muchanyo anasimulia jinsi ambavyo wamekuwa wakiteseka.

Anasema wamekuwa wakilala nje na kuna wakati mwingine wanakaa siku kadhaa na hata wiki kadhaa bila kufanya kazi.

Muchanyo, amekuwa nchini Afrika Kusini kwa miezi mitatu sasa, anasema ni bora kulala mitaani ambako maisha yake yatakuwa salama badala ya kulala ndani ya nyumba ambako maisha yake yatakuwa hatarini.

Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa kutoka nchini Zimbabwe ambaye anaishi mjini Johannesburg tangu Septemba mwaka 2007,Raymond Chingoma, anabainisha kuwa kuna watu wengi tu wenye uwezo wa kuifanya Zimbabwe kuendelea.

Lakini anasema tatizo lililopo linalochangia raia wengi kuteseka, linasababishwa na mtu mmoja tu Rais Robert Mugabe ambaye ameng'ang'ania madarakani kwa muda mrefu sasa .

Zimbabwe imekuwa katika wakati wa machafuko kwa kipindi cha zaidi ya mwezi sasa huku watu wote wakisubiri matokeo ya uchaguzi ambao kwa mara nyingine tena uliwashindanisha Rais Mugabe na Morgan Tsvangirai.Uchaguzi huo ulifanyika Machi 29, mwaka huu.

Hatimaye Ijumaa wiki iliyopita Maofisa wa Tume ya Uchaguzi nchini humo walikiri kuwa hakuna hata mmoja kati ya watu hao wawili aliyeshinda kwa zaidi ya asilimia hamsini ya kura, hali hiyo inafanya kuwepo na duru ya pili ya uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika wiki tatu zijazo.

Kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, kuliwafanya Athuar Mutambara aliyekuwa amejitenga na chama cha Movement for Democratic Change MDC, kuungana na kiongozi wa chama hicho Morgan Tsvangirai kwa lengo la kuongeza uwakilishi katika Bunge ili kuweza kumshinda Rais Robert Mugabe na Chama chake cha ZANU-PF ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka ishirini na nane.

Mugabe, ambaye waangalizi wa uchaguzi uliofanyika nchini humo mwaka 2002, wanasema aligeuza matokeo na kujitangaza mshindi huku wengine wakiamini kuwa Tsvangirai ndiye aliyekuwa mshindi.

Hivi sasa rais huyo anashutumiwa kwa kutumia Serikali na chama chake kuwatesa watu wote ambao hawamuungi mkono.

Vitendo ambavyo vimekuwa vikifanywa na polisi wa nchi hiyo dhidi ya raia katika operesheni yake, mwaka 2005 taarifa ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa vilisababisha zaidi ya watu lakini saba kukosa makazi.

Kwa upande wake Kundi la kutetea haki za binadamu nchini Zimbabwe la Sokwanele, linaifananisha hali iliyoko Zimbabwe kama kile kilichotokea kwa Wayahudi mwaka 1939, kilichofanywa na Manazi wa Ujerumani.

Hata hivyo wakimbizi wengi wanasema hawapati huduma bora zaidi. Chingoma anasema nchini Afrika Kusini wamekuwa hawachukuliwi kama binadamu bali kama wanyama.

Anasema wanapokwenda kuomba kufanya kazi sehemu yoyote hawapati na wanawaona wao kama siyo majirani zao na wala siyo Waafrika hivyo wanapaswa kuteseka japo kuwa anasema kitendo hicho siyo cha haki kwao.