1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Ujerumani wapendelea uchaguzi mpya

Mohammed Abdul-Rahman22 Novemba 2017

Baada ya Kansela Angela Merkel kushindwa kufikia makubaliano ya kuundwa serikali ya muungano na vyama vingine viwili, Wajerumani wengi sasa wanapendelea uchaguzi mpya kufanywa.

https://p.dw.com/p/2o2cw
Berlin Angela Merkel & Frank-Walter Steinmeier | Übergabe Entlassungsurkunde
Picha: Imago/photothek

Utafiti wa kura ya maoni uliochapishwa leo unaonesha nusu ya Wajerumani wanapendelea uchaguzi mpya baada ya Kansela Angela Merkel kushindwa kufikia makubaliano ya kuundwa serikali ya muungano na vyama vyengine viwili. Sehemu ndogo tu ya waliohojiwa ndiyo wanaounga mkono paweko na serikali ya wachache.

Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Masuala ya Jamii, INSA, kwa ajili ya gazeti la Bild unaonesha asilimia 49.9 ya Wajerumani wanapendelea uchaguzi mpya. Halikadhalika unaonesha asilimia 48.5 wanadhani chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic, SPD, kiko sahihi kukataa kujiunga katika serikali kuu ya mseto pamoja na wahafidhina wanaoongozwa na Bibi Angela Merkel. Ni asilimia 18 tu wanaopendelea paweko na serikali ya vyama hivyo vikubwa.

Mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano yalivunjika bila mafanikio hali ambayo imeiweka Ujerumani katika uwezekano wa kufanyika uchaguzi mpya
Mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano yalivunjika bila mafanikio hali ambayo imeiweka Ujerumani katika uwezekano wa kufanyika uchaguzi mpyaPicha: Reuters/A. Schmidt

SPD kilipata matokeo mabaya kabisa katika uchaguzi wa Septemba 24 kuwahi kushuhudiwa tangu 1949, baada ya kuwa katika serikali ya muungano iliyoongozwa na Kansela Merkel miaka minne iliyopita.

Kushindwa kwa mazungumzo baina ya kundi la wahafidhina la CDU/CSU la Merkel, chama cha FDP kinachopendelea wafanyabiashara na kile cha Kijani cha walinzi wa mazingira, kumeitumbukiza Ujerumani katika hali ya kisiasa ya kutatanisha na kuzusha uwezekano wa kuitishwa uchaguzi mpya.

Lawama kwa Lindner, Merkel na Ozdemir

Utafiti wa maoni unaonesha asilimia 28 wanamlaumu kiongozi wa FDP, Christian Lindner, kwa  kushindwa mazungumzo hayo, asilimia 27 wanamlaumu Merkel wakati  asilimia 13 wanamtwika lawama kiongozi wa chama cha kijani ,Cem Ozdemir.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Wanne katika jumla ya kila watu 10 waliohojiwa wanasema Merkel anapaswa kugombea tena ukansela ikiwa uchaguzi mpya utaitishwa, wakati asilimia 24 wangependelea paweko na mgombea mwengine kwa chama cha  Christian Democratic, CDU, ingawa hakuna maridhiano ya kutosha, nani awe mgombea badala ya Merkel.

Kuhusu kuundwa serikali baada ya uchaguzi mpya, wengi wanapendelea serikali ya muungano wa CDU na FDP na kufuatiwa na muungano baina ya SPD, chama cha kijani na kile cha mrengo wa kushoto, Die Linke. Hata hivyo, kuna maoni kwamba uchaguzi mpya hautobadili sana matokeo ya ule wa Septemba mwaka huu na hali hiyo kurejesha uwezekano wa kilichopo hivi sasa - yaani ama serikali iundwe na kati ya CDU/CSU na SPD au baina ya CDU/CSU, FDP na chama cha Kijani.

Wito wa Rais Frank-Walter Steinmeier

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amewataka wanasiasa waliohusika na mazungumzo yaliyovunjika kufikiria tena misimamo yao na umuhimu wa haja ya kufikia makubaliano. Ameshakutana na viongozi wa FDP na wa chama cha Kijani na anapanga kuonana hapo kesho (Alhamisi) na kiongozi wa SPD, Martin Schultz, ambaye amerejea tena kauli yake kwamba SPD kitabakia kwenye upinzani, msimamo unaoungwa mkono pia na chama chake.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef