Raia wa Uholanzi wapinga hatua za kukaa karantini
26 Januari 2021Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte amewaambia waandishi wa habari kuwa ghasia hizo hazikubaliki na kwamba zitazidi kuwatia watu hofu. Kuanzia usiku wa Jumatatu, waandamanaji waliingia mabarabarani kwenye miji kadhaa baada ya serikali ya Uholanzi kutangaza karantini kwa ajili ya kuzuia kuongezeka maambukizi ya virusi vya corona mwishoni mwa wiki.
Polisi walipambana na waandamanaji katika mji mkuu wa Amsterdam na katika mji wa bandari wa Rotterdam, ambapo watu wenye hasira walivunja vioo vya maduka, na polisi walitumia maji ya washawasha kuwatawanya waandamanji hao.
Vurugu pia zilitokea nchini Israeli, ambapo basi lilichomwa moto kwenye eneo moja la maandamano ya kupinga hatua za kudhibiti maambukizi yaliyofanyika katika wilaya za Ultra-Orthodox, Bnei Brak karibu na Tel Aviv, na Mea Shearim katika jiji la Jerusalem.
Na huko nchini Australia, maelfu ya watu wameandamana leo Jumanne kupinga sheria za kudhibiti maambukizi ya corona.
Mbali na hayo mvutano juu ya usambazaji wa chanjo za COVID -19 umeibuka katika siku za hivi karibuni. Kampuni ya AstraZeneca inayotengeneza chanjo ya COVID 19 kwa ushirikiano wa Uingereza na Uswisi inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya baada ya kampuni hiyo kutangaza wiki iliyopita kwamba haitaweza kusambaza chanjo kama ilivyopangwa. Hatua hiyo imelaumiwa vikali na waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn. Chanjo hiyo a AstraZeneca bado inahitaji kupitishwa rasmi nan chi za Umoja wa Ulaya ambapo uamuzi huo unatarajiwa kutangazwa siku ya Ijumaa.
Matatizo yanayoendelea kujitokeza kuhusu usambazaji wa chajo za COVID -19 bila shaka yanakwamisha kampeni ya kutoa chanjo katika nchi za Jumuiya ya Ulaya. Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn ameiambia DW kwamba anaunga mkono ufuatiliaji wa karibu wa kiwango kinachopelekwa nje cha chanjo zinazotengenezwa na Umoja huo.
Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limetahadharisha juu ya kuziacha nyuma nchi masikini katika ugavi wa chanjo likisisitiza kwamba kushindwa kuzingatia usawa katika ugavi kutasababisha hasara ya matrilioni ya dola kwenye uchumi wa dunia.
Umoja wa Mataifa unesena janga la corona linasababisha ukosefu wa ajira, Shirika la Kazi Duniani (ILO) limesema hasara hiyo inawakilisha nafasi za ajira milioni 255 mara nne zaidi ya nafasi za ajira zilizopotea mnamo mwaka 2009 wakati wa mgogoro wa fedha ulioikumba dunia nzima.