1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Raia wa Sudan wazidi kuyakimbia mapigano

Sylvia Mwehozi
26 Juni 2023

Wanamgambo wa kundi la RSF la nchini Sudan, wanasema wanakishikilia kituo kikubwa cha polisi kilichokuwa na silaha nzito wakati wa mapiganao makali baina yake na jeshi huku watu takribani 12 wakiuawa mjini Darfur.

https://p.dw.com/p/4T37U
Mzozo wa Sudan
Raia wakikwea lori kukimbia KhartoumPicha: AP/picture alliance

Katika taarifa yake, kundi la wanamgambo la RSF, limesema kwamba limechukua udhibiti kamili wa kituo cha polisi wa akiba kusini mwa Khartoum na kuchapisha video za wapiganaji wake wakisherehekea ndani ya kituo, baadhi wakiondoa masanduku ya risasi kutoka kwenye ghala. Tangu Jumamosi jioni mapigano yameripotiwa kuongezeka katika miji mitatu ya Khartoum, Bahri na Omdurman huku mzozo kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF ukiingia wiki ya 11.

Mashuhuda wameripoti pia ongezeko la machafuko kwenye mji mkubwa wa Nyala katika mkoa wa magharibi wa Darfur kama anavyosimulia raia huyu wa Sudan; "Tunatumai kuwa vita hivi vitaisha. Watu wameumizwa vibaya sana kutokana na vita hivi. Baadhi wamekimbia nyumba zao na wengine wamekwama mipakani. Tunaamini kwa msaada wa Mungu vita hivi vitakomeshwa.”

Umoja wa Mataifa ulitoa tahadhari siku ya Jumamosi kwamba ghasia za Darfur zimechukua "mwelekeo wa kikabila" na zinaweza kujumuisha "uhalifu dhidi ya ubinadamu", na kuonya juu ya mauaji ya watu kutoka jamii ya Masalit katika eneo la El Geneina Darfur Magharibi. Khartoum na El Geneina ni maeneo yaliyoathirika vibaya na vita, ingawa wiki iliyopita mapigano yalienea katika maeneo mengine ya Darfur na Kordofan upande wa kusini.

Sudan Khartoum| Omdurman
Picha ya kutoka angani ikionyesha moshi ukifuka kutoka katikati mwa OmdurmanPicha: REUTERS

Umoja wa Mataifa umehimiza "hatua za haraka" za kukomesha mauaji ya watu wanaokimbia El Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi, mauaji yanayofanywa na wanamgambo wa Kiarabu wakisaidiwa na wanamgambo wa RSF. Mapigano yamepamba moto tangu mkururo wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoongozwa na Marekani na Saudi Arabia mjini Jeddah kumalizika.

Jeshi linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan, limekuwa likitumia mashambulizi ya anga na mizinga mikubwa kujaribu kuwatimua wanamgambo wa RSF walio chini ya Mohamed Hamdan Daglo, kutoka vitongoji vya mji mkuu wa Khartoum. Hayo yakiarifiwa, watu takribani 12 wanaripotiwa kuuawa kwenye mapigano mjini Darfur. Taarifa hizo zimetolewa na Daktari mmoja aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa masharti ya kutotajwa majina, akiongeza kuwa machafuko yanayoendelea yanawazuia wahanga kuweza kufika hospitali. 

Soma hii pia: Maelfu wakimbia mapigano Kordofan Kusini

Takriban watu 2,800 wameuawa nchini Sudan tangu mapigano yalipoanza katika mji mkuu Khartoum Aprili 15, kulingana na takwimu mpya za mashirika yanayofuatilia vita hivyo. Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema kwamba watu wengine milioni mbili wamekuwa wakimbizi wa ndani na takriban 600,000 wamekimbia nje ya mipaka ya Sudan.

Vyanzo: (Reuters/AFP)