Raia wa Mali wajiandaa kuipigia kura rasimu ya katiba
15 Juni 2023Raia nchini Mali wanajitayarisha kuipigia kura rasimu ya katiba inayopendekezwa na utawala wa kijeshi wa taifa hilo ikiwa ni zoezi la kwanza la kidemokrasia kuandaliwa na utawala huo uliotwaa madaraka mnamo Agosti 2020.
Zoezi la kupiga kura litafanyika siku ya Jumapili kuanzia saa mbili asubuhi na wale wanaoshiriki watatumia karatasi za rangi ya kijani kuunga mkono au nyekundu kuipinga rasimu hiyo ya katiba. Mali yashindwa kulipa madeni yake
Kura hiyo imepangwa licha ya taifa hilo kuendelea kuandamwa na mizozo ikiwemo hali dhaifu ya usalama na uchumi unaochechemea. Watawala wa kijeshi wanaipigia upatu rasimu hiyo kama msingi wa mageuzi kwa matatizo yaliyotokana na katiba ya Mali iliyoandikwa mwaka 1992.
Inatarajiwa katiba hiyo itakuwa hatua ya mwanzo kuelekea mipango ya jeshi kuachia madaraka na kulirejesha taifa hilo chini ya utawala wa kiraia hapo Machi mwaka 2024.