Raia wa DRC na Libya wapewa tuzo
14 Agosti 2012Wanaharakati hao, pamoja na washindi wengine wanne, watakabidhiwa tuzo yao mwezi Novemba mwaka huu, katika hafla maalum iitwayo „Sauti za Haki.“ Tuzo hiyo ya shirika la Human Rights Watch imepewa jina la Alison Des Forges ikimuenzi mwanamke aliyekuwa mkuu wa kitengo cha Afrika katika shirika hilo mjini New York, Marekani. Alikuwa mtaalamu wa masuala yahusuyo Rwanda na alijishughulisha zaidi na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na athari zake. Tuzo yake inawaenzi watu wanaopambana na unyanyasaji, ubaguzi na ukandamizaji.
Akizungumza na DW, mshindi wa tuzo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Padri Abbé Benoit Kinalegu alielezea furaha yake ya kupokea tuzo hiyo: "Ni jambo linalonipa moyo , linanipa motisha na kuwapa motisha watu wangu, kwambani mmoja kati ya watoto wao anayetumia muda wake usiku na mchana kutetea haki za binaadamu hapa mahali nilipo."
Kupitia taarifa katika redio, Kinalegu alikuwa akiwaarifu watu juu ya maovu yanayofanywa na kundi la waasi wa Lord's Resistance Army, LRA. Aliundda pia mtandao uliowawezesha raia kuripoti juu ya mavamizi yanayofanywa na waasi. Mbali na hayo, Padri Kinalegu anawasaidia wahanga wa maasi ya LRA kurejea katika maisha ya kawaida. Watu hao ni wale waliotekwa na waasi na baadaye kufanikiwa kutoroka.
Wangari Maathai aliwahi pia kupokea tuzo
Kinalegu na Salah Marghani, ambaye ni mshindi wa tuzo kutoka nchini Libya, watapokea tuzo zao nchini Marekani. Miongoni mwa mengine, Kinalegu atatembelea Silicon Valley na mji wa Santa Barbara huku Marghani akisafiri kuelekea Beirut, mji mkuu wa Lebanon.
Akielezea madhumuni ya ziara hizo, Winky Worden wa shirika la Human Rights Watch alisema: "Tunachofanya ni kuwapa nafasi wanaharakati hao, ambao wengi wanahatarisha maisha yao, kuzungumzia hali ilivyo katika nchi wanazotoka. Tunawapa pia nafasi ya kukutana na wanahabari na kuzungumza na wanasiasa wenye nguvu ya kumaliza unyanyasaji."
Baadhi ya washindi wa Tuzo ya Alison des Forges baadaye walipokea pia tuzo ya amani ya Nobel. Miongoni mwao ni marehemu Wangari Maathai kutoka Kenya na msanii Liu Xiaobo kutoka China
Mwandishi: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman