Raia wa Benin wamchagua rais mpya
6 Machi 2016Raia wa Benin wamejitokeza kupiga kura leo kumchagua rais mpya, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu usambazaji wa kadi za kupigia kura ambao tayari uliuchelewesha uchaguzi huo kwa wiki mbili. Upigaji kura umeanza mwendo wa saa 12 asubuhi katika taifa hilo dogo la Afrika Magharibi, huku waangalizi wa kimataifa wakiyatathmini mazingira ya uchaguzi kuwa ya utulivu. Upigaji kura unatarajiwa kukamilika baada ya saa tisa.
Mathieu Boni, afisa wa kundi moja la kijamii ambalo limewatuma zaidi ya waangalizi 3,000 wa uchaguzi, alisema zaidi ya nusu ya vituo karibu 8,000 vilifunguliwa kwa wakati uliotakiwa.
Rais Thomas Boni Yayi anaondoka madarakani baada ya kuhudumu awamu mbili za miaka mitano, akijiepusha kuingia katika orodha ya baadhi ya viongozi wa Afrika ambao wamejaribu kuzibadili katiba kuhakikisha wanapata awamu ya tatu ya kuongoza. Matokeo ya kwanza yanatarajiwa kutolewa katika kipindi cha masaa 72.
Wagombea mashuhuri ni Lionel Zinsou, mtaalamu wa fedha raia wa Benin na Ufaransa, aliyejiuzulu kama mkuu wa benki ya uwekezaji ya Ufaransa kuwa waziri mkuu wa Benin mwaka uliopita. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 anagombea urais kupitia tiketi ya chama tawala, Cowry Forces for an Emerging Benin, FCBE, na anaonekana kwa kiwango kikubwa kama mrithi aliyechaguliwa na Boni Yayi. Hata hivyo Zinsou kuwa uraia wa nchi mbili huenda kukamuathiri huku wengine wakidai ameletwa ili kutimiza masilahi ya mkoloni wa zamani Ufaransa.
Uungwaji mkono wa vyama vikubwa
Zinsou tayari anaungwa mkono na vyama viwili vya upinzani lakini wakosoaji wanamuona kama mtu kutoka nje ambaye hana umaarufu na aliyeingizwa na mkoloni wa zamani wa Benin, Ufaransa. Zinsou, ambaye katika miaka ya 1980 alikuwa mwandiahi wa hotuba za waziri mkuu wa zamani wa Ufaransa, Msoshalisti Laurent Fabius, alipiga kura muda mfupi kabla saa sita mchana katika eneo la Cocotiers la mji mkuu Cotonou.
Wafanyabiashara wawili mashuhuri, Patrice Talon, mwenye umri wa miaka 57, na Sebastien Ajavon, mwenye umri wa miaka 51, pia ni wagombea wanaowania urais baada ya kushindwa katika chaguzi za awali.
Wagombea wengine mashuhuri ni pamoja na mwanauchumi na afisa wa zamani wa shirika la fedha la kimataifa, IMF, Abdoulaye Bio Tchane, aliyepewa jina la ABT na wafuasi wake, na waziri mkuu wa Pascal Irenee Koupaki, wote wakiwa na umri wa miaka 64, ambao wamepiga kura katika mji wa kaskazini wa Djougou na mji wa kusini wa Pomasse.
Huku wagombea 33 wakishiriki katika kinyang'anyiro cha kuwania urais, wachambuzi wanabashiri matokeo hayatatao mshindi wa moja kwa moja na wanaamini atakayeshinda katika eneo la kaskazini ataamua matokeo jumla.
Changamoto katika sekta ya kiuchumi
Kazi muhimu ya rais anayekuja ni kuimarisha uchumi wa Benin, taifa linalotegemea sana kilimo na ambalo husafirisha sana korosho na siagi kwa wingi nje ya nchi. Masuala muhimu katika uchaguzi wa mwaka huu ni kutengeneza nafasi za ajira, kupambana na rushwa, kuboresha sekta ya afya na elimu na uchumi, katika taifa hilo ambalo ni mzalishaji mkubwa wa zao la pamba.
Mkulima Emile Sosa alikuwa miongoni mwa watu waliopiga kura kwanza katika eneo la Cocotiers jijini Cotonou na anasema kukosekana fursa kwa vijana wa Benin ni tatizo kubwa. "Ninataka rais anayekuja awatie moyo vijana wajiingize katika kilimo," alisema baba huyo wa watoto wanne mwenye umri wa miaka 49.
Duru ya kwanza ya kupiga kura ilikuwa imepangwa kufanyika Februari 28 lakini ikaahirishwa kwa sababu ya kuchelewa kutengenezwa na kusambazwa kadi za kupigia kura milioni 4.7. Jumamosi jioni, usambazaji wa kadi mpya za kupigia kura ulikuwa haujaanza katika majimbo mawili ya katikati mwa nchi - Zou na Plateau - na ulikuwa haujakamilika katika majimbo kadhaa kati ya majimbo mengine 10 ya taifa hilo.
Mkuu wa tume huru ya uchaguzi, Emmanuel Tiando, amewaambia waandishi wa habari kwamba kadi za zamani na mpya za kupigia kura zingeweza kutumika leo kuepusha hali ya wasiwasi na kuwaruhusu wapigaji kura kushiriki katika upigaji kura. "Katika majimbo ya Zou na Plateau, upigaji kura utaruhusiwa na vitambulisho badala ya kadi za kupigia kura," aliongeza kusema Mkuu wa tume ya uchaguzi, huku akisisitiza kwamba vifaa vya kupigia kura vilikuwa vimeshapelekwa katika vituo vya kupigia kura kote nchini.
Mpigaji kura Franck Tokannou alisema baada ya kupiga kura mjini Cotonou, "Asubuhi hii imekuwa ngumu kwa wale wanaoratibu uchaguzi, lakini inaonekana mambo yanakwenda vizuri. Kila kitu kiko sawa."
Mwandishi:Josephat Charo/afpe/ape/rtre
Mhariri:Sudi Mnette