Raia mwingine auawa katika maandamano ya Khartoum
31 Januari 2022Tume ya madaktari wa Sudan imethibitisha juu ya kifo cha mwandamanaji mmoja aliyekuwa na umri wa miaka 27 na kwamba aliuawa mjini Khartoum akiwa na jeraha kifuani. Waandamanaji kadhaa walionekana wakipata shida ya kupumua na kuvuja damu baada ya kupigwa na mabomu ya kutoa machozi. Takriban watu 79 wameuawa na mamia kujeruhiwa katika msako wa maandamano ya kupinga mapinduzi, kulingana na kundi huru la madaktari.
Maandamano ya Jumapili pia yalifanyika katika maeneo mengine yakiwemo miji ya kaskazini ya Atbara na Dongola, na huko Darfur magharibi mwa nchi. Mjini Khartoum, vikosi vya usalama vilifunga madaraja muhimu na barabara zinazoelekea kwenye ikulu ya rais. Kulingana na wanaharakati, watu takribani 45 walikamatwa na mamlaka kabla ya maandamano ya Jumapili. Mamlaka za Sudan mara kwa mara zimekanusha kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji, na kusisitiza kuwa maafisa wengi wa usalama wamejeruhiwa. Jenerali mmoja wa polisi aliuawa kwa kuchomwa kisu wakati wa machafuko hayo mapema mwezi huu.
Chama cha wanataaluma wa Sudan, ambacho ni mwavuli wa makundi yaliyoongoza maandamano ya kumpinga Omar al Bashir na baadaye maandamano ya kupinga mapinduzi, kimeapa kuwa maandamano hayo hayatakoma. "Hatutaondoka mitaani hadi kuanguka kwa utawala wa mapinduzi, kurejesha serikali ya kidemokrasia na kuwawajibisha wauaji wote na wale waliofanya uhalifu dhidi ya watu," ilisema taarifa ya chama hicho kabla ya maandamano ya Jumapili. Waandamanaji 7 wauawa na vikosi vya usalama Sudan.
Sudan, ambayo tayari ilikuwa katika hali mbaya ya mzozo wa kiuchumi kabla ya mapinduzi, imeshuhudia misaada muhimu ya kigeni ikisitishwa kama sehemu ya jumuiya ya kimataifa kulaani mapinduzi ya kijeshi.
Umoja wa Mataifa, ambao hivi karibuni ulianzisha mazungumzo kati ya pande zinazozozana katika jitihada za kutatua mzozo wa baada ya mapinduzi, umeonya mamlaka za Sudan dhidi ya kutumia nguvu kuzima maandamano ya kisiasa. Marekani nayo imeonya kwamba ukandamizaji unaoendelea utakuwa na athari kubwa.
Jenerali mwenye nguvu Mohammed Hamdan Dagalo, ambaye ni naibu mkuu wa Baraza kuu linalotawala, amedokeza juu ya kukubaliana na juhudi za Umoja wa Mataifa za kutatua mgogoro huo.